Ijumaa. 03 Mei. 2024

Mt. Ambrosi wa Milano

Ambrosi wa Milano

Ambrosi mtoto wa gavana wa Ufaransa, alizaliwa Tria (Trier, Ujerumani) mnamo mwaka 340 katika familia ya waroma. Siku moja alipokuwa bado mtoto, aliwasindikiza mama yake na dada yake kwenda kanisani. Walipofika kanisani aliona wakibusu mkono wa askofu. Mara alisema: "Ubusuni mkono wangu pia, kwa sababu nami nitakuwa askofu". Alipomaliza masomo yake ya sheria huko Roma (Italia) Kaisari alimweka kuwa gavana wa Italia ya Kaskazini, akaishi huko Milano. Alipokufa askofu wa Milano, aliyekuwa adui na mfitini wa Arios, wakristu waligombana na wafitini hata karibu kupigana. Ndipo gavana Ambrosi alipokuja kuzizima kelele zile za watu. Aliwaambia watulie mpaka atakapochaguliwa askofu mwingine. Alipokuwa akisema vile mara mtoto mmoja akalia: "Ambrosi ndiye askofu", na watu walianza kukariri hivyo.

Kwanza Ambrosi alikataa, akatoroka wakati wa usiku, lakini mwisho ilimpasa akubali. Kwa sababu alikuwa hajabatizwa bado, alibatizwa kwanza; siku nane zilizopita ndipo akapewa uaskofu, 7 Desemba mwaka 374.

Ambrosi aliwagawia maskini mali zake, na alianza kusoma Maandiko Matakatifu. Aidha aliwarudisha wafitini wengi wa dini kwenye imani Katoliki, na hasa alimwomba Mt. Augustino, aliyekuwa baadaye mwalimu mkuu wa kanisa la Afrika.

Zamani zile Kaisari Teodori aliamuru watu wa Tesalonika (Ugiriki) walioiasi serikali waadhibiwe, hivyo watu elfu saba wakauawa. Askofu Ambrosi aliposikia hayo, alipatwa na hasira. Alikusudia kuwaangamiza watu hao waliomwaga damu ya watu wengine. Alipopata habari kwamba Kaisari alitaka kuja kanisani kushiriki katika misa, Ambrosi akivaa mavazi yake ya kiaskofu, akamngojea kwenye mlango wa kanisa. Teodori alipotaka kuingia, Ambrosi alimzuia akasema kwamba hawawezi kumpa ruhusa ya kuingia kanisani mtu aliyechafuka kwa damu ya watu. Kaisari alizidi kumwomba askofu akisema ya kuwa mfalme Daudi naye alikuwa amekosa. Askofu Ambrosi akamjibu: "Basi, kama umemfuata Daudi katika kosa lake, mfate pia katika kitubio chake". Teodori alikubali akatimiza malipizi aliyopewa na Ambrosi. Mtakatifu Ambrosi ni mwalimu wa kanisa, kwani aliandika vitabu kwa kuwaonyesha wakristu njia ya kwenda mbinguni, na kwa kuilinda Imani Katoliki, hasa kwa kuupinga uzushi wa Arios. Alikufa siku ya Jumamosi Kuu, 4 Aprili mwaka 397.

Maoni


Ingia utoe maoni