Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Nikola, Askofu Wa Miri

Nikola, Askofu Wa Miri

Mtakatifu Nikola ndiye mmoja wa maaskofu wa Mashirika anayesifiwa zaidi. Alizaliwa katia Asia ndogo (Uturuki). Hatujui historia ya maisha yake, ila alikuwa askofu wa Mira (Uturuki) na katika karne ya sita lilikuwepo kanisa la Mt. Nikola mjini Konstantinopoli. Kisha karne ya tisa huko Mashariki, na kisha karne ya kumi na moja huko Magharibi ibada yake imeenea sana. Alitajwa somo wa mabaharia, kadhalika wa watoto, wafanya biashara na wengineo. Mtakatifu Nikola ni mmojawapo wa watakatifu walioheshimiwa sana katika nchi nyingi.

Iko hadithi isemayo kwamba tajiri mmoja alikuwa amepoteza mali zake zote. Kwa kuwa hakuwa na kitu tena, alifanya shauri moyoni mwake kuwafanya binti zake watatu wawe malaya. Mtakatifu Nikola alipopata habari hii aliutupa mfuko wa fedha katika dirisha la nyumba ya mtu huyo, ili akawaposeshe binti zake.

Mjomba wake Nikola aliyekuwa askofu mkuu wa Mira, alimpa upadre. Baadaye Nikola alisafiri kwenda kuizuru nchi takatifu. Alipokufa askofu wa Mira, maaskofu wengine walitaka kumchagua askofu mwingine, basi wakasemezana: "Atakayeingia kanisani kesho asubuhi wa kwanza, ndiye atakayeteuliwa na Mungu". Kulipokucha, Nikola alikuwa wa kwanza kuingia humo kanisani, na mara aliwekwa kuwa askofu wa Mira.

Alikuwa akifunga kila siku, hakula nyama wala kunywa divai. Usiku alilala juu ya kirago au mbao. Aliamka asubuhi sana ili apate kuimba nyimbo za zaburi pamoja na mapadre wengine. Akafa Mira, lakini mwili wa askofu huyu ulizikwa kwanza Mira, alafu ulihamishiwa Bari (Italia), ambapo unaheshimiwa na wakristu mpaka hivi leo.

Maoni


Ingia utoe maoni