Saba (Sabbas) Mkaa Pweke
Mtakatifu Saba alizaliwa mwaka 489 katika kijiji kilicho karibu na Kaisari (Israeli) Baba yake alikuwa ofisa katika jeshi la Waroma, akahamishwa mara kwa mara, na kila mara alikuwa akifuatana na mkewe. Kwa hivi, mtoto Saba alikuwa akiachwa nyumbani akiwa mikononi mwa ndugu ambao walikuwa mawakala wa mzee wake waliokuwa na jukumu la kuyatunza mashamba yake makubwa. Lakini saba alikuwa hana raha hata kidogo, na kwa hivyo, alipoanza kukua, siku moja alitoroka nyumbani, akakimbilia kwenye monasteri iliyoko kijijini. Kuna usemi kwamba, licha ya umri wake mdogo, alikuwa na bidii za kiroho zilizokuwa kubwa ajabu kiasi cha kuzipata hata zile za watu wengine waliomzidi kwa umri.
Alipotimiza umri wa miaka kumi na minane, aliamua kuhama kufuatana na kusudio lake la kuishi maisha ya upweke. Lakini yule mkaa pweke ambaye alitaka amwongoze, yaani, mtakatifu Eutimi, alimwomba Saba angali kijana mno kwa kuishi maisha ya upweke, akamshauri akae kwanza kwa muda mrefu zaidi monasteri. Basi, Saba akalikubali shauri la huyo kiongozi wake. Akiwa katika monasteri, alijitolea kwa moyo wake wote kuishi maisha bora ya kiroho na kuyatekeleza mapenzi ya Mungu yaliyomjia kwa njia ya wakuu wake. Hatimaye, alipoufikia umri wa miaka thelathini, alikubaliwa na Mt. Eutimi kuishi kama mkaa pweke na kuongozwa naye. Mtakatifu huyo alipofariki dunia, Saba akaenda kukaa jangwani katika pango kwa muda wa miaka minne. Alikuwa akila majani ya mimea iliyoliwa, na alikuwa akiletewa matunda na mkate na watu waliokuja kumtembelea.
Baada ya muda, aliona heri awakubali na wakaa pweke wengine ili waje nao kuishi karibu na pale anapoishi yeye, kusudi apate kuwaongoza. Kila mmoja wao alikaa peke yake kabisa katika nyumba zilizojengwa kulizungukia kanisa. Polepole idadi yao iliongezeka, hata ikakaribia mia moja hamsini. Baadhi yao hawakuridhika sana kwa sababu miongoni mwao, hakuwepo hata mmoja aliyekuwa padre, wakamlalamikia hata askofu mkuu wa Yerusalemu kuhusu jambo hilo. Baada ya kufanya utafiti, askofu huyo alimlazimisha Saba apadirishwe, katika mwaka 491.
Sifa za maisha yake matakatifu zilivuma sana kiasi cha kuwavuta kwake watu wengi, sio tu wale waliokuwa wakiishi karibu yake, bali hata wale waliokuwa wakiishi mbali naye. Baada ya kufiwa na mumewe, hata mama yake mwenyewe, alitamani kumtumikia Mungu akiwa chini ya uongozi wake. Fedha alizozileta mama yake, zilimsaidia Saba kujengesha monasteri nyingine, kadhalika, hospitali tatu.
Mwaka 511, Elias askofu mkuu wa Yerusalemu, alimwita abati Saba, ambaye alikuwa sasa na umri wa miaka sabini, ili awe mjumbe wake. Alimtuma Konstantinopoli (Uturuki) kwa Kaisari amsihi, kwa mkazo, awatiishe wafitini wenye kuyatangaza mafundisho ya uwongo kila mahali, badala ya kuwadhulumu wakristu wale waliokataa kuyakubali mafundisho hayo. Hali ya Mtakatifu ya mzee abati Saba ilimchoma moyo Kaisari, lakini, hata hivyo, hakuibadili nia yake.Kinyume chake, alimkasirikia sana askofu mkuu Elias, akamfukuza mjini Yerusalemu. Miaka ishirini hivi baadaye abati mzee Saba alisafiri tena kwenda Konstantinopoli ili kuwaombea na kuwatafutia msaada watu wa Palestina waliokuwa wameteswa sana siku za vita. Muda mfupi baada ya kurudi katika monasteri yake, alifariki dunia. Alikuwa na miaka tisini na minne.
Mt. Saba ni mmonaki aliye maarufu sana wa karne za kwanza kwanza za kanisa. Tunashangazwa hasa na juhudi zake kubwa alizozifanya katika kuishi maisha ya kiroho, pamoja na moyo wake wa kuyakubali mapenzi ya Mungu kila mara alipoyatambua, hata alipokuwa mzee.
Kuna hadithi moja ambayo hutuonyesha heshima aliyokuwa nayo, kama mtu wa Mungu aishiye katika muungano dhabiti na Mungu. Siku moja Mtakatifu Saba alitaka kwenda kutawa pangoni alimokuwamo Simba mkali. Simba huyo alipomwona mkaa pweke huyo, hakumrukia, bali alimvuta taratibu kwa upindo wa nguo yake kama vile angetaka kusema: Ondoka hapa. Lakini, Mt. Saba, bila wasiwasi alianza kusali sala zake za asubuhi,simba alikuwa amesimama kimya na kumtazama tu. Mt. Saba alipokwisha sali, Simba akaivuta nguo yake kwa mara ya pili. Ndipo Mt. Saba alipomwambia kwa upole: "Naona humu pangoni imo nafasi kwa sisi sote wawili, lakini kama ukipenda kaa peke yako, nenda zako, kwani mnyama wa mwituni hampiti mtumishi wa Mungu". Baadaya ya kuyasema hayo maneno, Simba akaenda zake wala hakurudi tena.
Maoni
Ingia utoe maoni