Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Yohani wa Damasko

Yohani wa Damasko

Yohani alizaliwa Damasko (Siria) na wazazi wakristu, mwisho wa karne ya saba. Zamani hizo, mji wa Damasko ulitawaliwa na Sultan Oman. Ingawa baba yake Yohani alikuwa mkristu, alikubaliwa na waislamu na akafanywa liwali kwa sababu ya haki na utaratibu wake. Yohana alipata elimu yake kwa mmonaki mmoja Mgiriki jina lake Kosma. Alipokufa baba yake, Yohani akafanywa liwali mahali pake. Alitoa hukumu kwa sifa ya raia wake, wala hakuna aliyemwonea. Alikuwa mwema na alionesha moyo wa usawa kwa watu wote, tena hakujivunia ingawa alikuwa mtu mkuu vile katika nchi, chini ya Sultani.

Wakati ule, Kaisari wa Roma jina lake Leo Msori alikuwa akiidhulumu dini. Yeye alisema: "Mtunza sanamu ni mwabudu sanamu". Basi, aliamuru sanamu takatifu zivunjwe. Watu hawakuruhusiwa kuwa na masanamu makanisani au majumbani kwao. Aliyeivunja amri hiyo, aliadhibiwa vikali. Walimu wengine, hasa Yohani wa Damasko, walimwandikia Kaisari nyaraka za kuzikanusha hoja zake. Kwa vile Yohani alikuwa chini ya serikali ya Waislamu, hakuwa raia wa Kaisari na hivi hakuweza kukumatwa na kufungwa kwa ajili ya msimamo wake huo. Akiwa bingwa katika falsafa na teolojia aliandika 'Imani ya Ortodoksi' mintarafu mafundisho ya Kanisa, hasa dhidi ya wale waliohimiza kuharibiwa sanamu takatifu. Kitabu hiki husomwa sana na Maaskofu na Wakristu popote duniani.

Kwa sababu alipenda kumtumikia Mungu zaidi, Yohani alijiuzulu kazi ya uliwali. Aliuza mali zake akawagawia maskini. Kisha akaingia umonaki katika monasteri ya Mt. Sabas (tazama 5 Desemba) karibu na Yerusalemu Israeli. Huko alikutana tena na mwalimu wake Kosma. Huyu alimshauri: "Usifuate mapenzi yake mwenyewe hata siku moja. Ujizoeze kujiona si kitu, usijipendekeze, usipende kiumbe chochote kwa ajili yake tu. Usiingize upendo wowote moyoni mwako, ila ule upendo wa kumpenda Mungu. Kila siku mtolee Mungu kazi zako, masumbuko na sala zako. Usijivune kwa sababu ya elimu yako wala kwa sababu yoyote ike. Ungama mbele ya Mungu ujinga na udhaifu wako. Kaa kimya ukijua ni hatari kufungua mdomo wako pasipo lazima, weka nia ya kuzungumza maneno mema".

Katika monasteri hiyo alipewa upadre. Daima alifanya kazi ngumu pamoja na wenzake, hakuchoka kusali na kumwaza Mungu. Alikuwa mnyenyekevu sana. Alitumia elimu yake ya teolojia katika kuandika vitabu vinavyoeleza mafundisho ya dini, kutunga nyimbo na pia kupinga wafitini wa dini waliosisitiza uvunjaji wa sanamu takatifu. Alikufa mwaka 749. Yohani wa Damasko alitajwa kuwa Mwalimu wa Kanisa, mwaka 1890.

Maoni


Ingia utoe maoni