Jumatatu. 06 Mei. 2024

Mt. Bibiana, Mfiadini

Bibiana, Mfiadini

Hatujui kwa hakika matokeo ya kufa kwake Bibiana, ila katika karne ya tano wakristu wa Roma (Italia) walikuwa na kanisa la Mfiadini Mt. Bibiana. Inasemekana kwamba alizaliwa Roma katika ukoo wa watu wenye cheo na heshima. Lakini jambo lililo muhimu zaidi ni kwamba asili ya ukoo huo ilikuwa ya kikristu, kwa kuwa wazazi wake, Flaviano na Dafrosa, walikuwa wafiadini, walioteswa na kuuawa na Yuliano aliyekuwa mkana dini. Wazazi wake walipokufa, yeye na dada yake Demetria walinyang'anywa mali zao zote. Walijaribiwa kwa mabembelezo na vitisho na liwali wa mji, ili waiache imani yao ya kweli. Lakini wakiwa hodari na imara waliuchukia upotofu wa liwali huyo.

Kuna hadithi ya kwamba Demetria alipofariki, liwali alimpeleka Bibiana kwa mwanamke mwasherati ilimradi ampevushe na kuuharibu ubikira wake, lakini hakifaulu hata kidogo. Kinyume chake, mwanamke yule alipouona uthabiti wa Bibiana, aliongoka naye akawa mkristu. Liwali aliposikia hayo aliingiwa na ghadhabu, akatoa amri Bibiana avuliwe nguo, wamfunge mikono na miguu, wampige fimbo. Alipigwa hata akazimia, mwisho akakata roho. Mwili wake ulitupiwa mbwa, nao hawakuugusa. Wakristu walikuja wakauzika mwili huo kwa heshima. Alikufa mwaka 363, wakati wa mateso yaliyoenezwa na Kaisari Yuliano mkana dini.

Maoni


Ingia utoe maoni