Jumatatu. 06 Mei. 2024

Mt. Eliji, Askofu

Eliji, Askofu

Eliji alizaliwa Limoges (Ufaransa) katika mwaka 588. Alikuwa Sonara, mfua dhahabu na kwa sababu ya umahiri wake mkubwa, sifa zake zilivuma mpaka zikafika barazani kwa Mfalme Klotari wa Pili. Mfalme huyu alimwagiza amfulie vitu vya johari zake, na amtengenezee sanduku la kuwekea masalia ya watakatifu. Kazi ya sanaa zake mbalimbali zimehifadhiwa mpaka hivi leo.

Eliji hakujivunia huo ufundi wake, bali alizidi kuwa mnyenyekevu, akisali na kufunga. Mshahara aliopata kwa kazi zake aliutumia kwa kuwakombolea watumwa, na pia kujenga monasteri huko Solinyak, na konveti mjini Paris katika nchi ya Ufaransa. Wageni walipokuwa wakiuliza mahali alipokuwa akikaa Mtakatifu Eliji, walijibiwa: "Fuateni njia hii, huko kundi zima la maskini wanakokaa, ndiko naye Fundi Eliji anakokaa". Watu walipoona ya kwamba Mungu amemjalia uwezo wa kuwaponya vipofu kwa ghafla, wakazidi kumheshimu.

Eliji akawa padre, na mtakatifu Akari, askofu wa Noyoni (Ufaransa), alipofariki, mapadre na wakristu wote, kwa kauli moja walimtaka Eliji awe askofu wao. Ingawa yeye mwenyewe hakupenda, ilimlazimu awe askofu. Eneo la jimbo lake lilikuwa kubwa sana. Alikuwa mhubiri hodari sana aliyewavutia wengi.

Alijionyesha kuwa askofu mwenye bidii katika kazi yake ya kiuchungaji kama ile juhudi aliyokuwa nayo hapo zamani katika kazi yake ya kufua dhahabu. Aliwahudumia maskini, aliwashauri wenye madaraka na uwezo, na aliendelea na kazi yake ya kuwakomboa watumwa kama vile alivyokuwa akifanya kabla hajawa padre. Aliwaongoa watu wengi sana katika nchi ya Ubelgiji, wakaifuata dini ya Yesu Kristu. Alizistawisha sana nchi hizo. Alijenga makanisa mahali pengi, ni yeye huyo aliyewahimiza Wafrisi (Uholanzi) kuyatengeneza mashamba ili yawe mazuri.

Aliporudi katika nchi yake, aliyapinga mazoea mabaya ya kipagani yaliyokuwa yamezagaa pote. Hapo ndipo hasa ulipojidhihirisha ule uwezo wake wa kuwa mhubiri stadi na kamwe hakuacha kusema kuhusu mazoea hayo maovu. Aliwasisitiza sana waumini wake waepukane kabisa na ile desturi ya ramli, kuwachunguza ndege kama wanatabiri ishara nzuri au mbaya, au kuifanya siku ya alhamisi iwe siku takatifu ya mungu Jupiter. Badala ya mambo hayo yote, wangejiimarisha kwa ishara ya msalaba, sala na hasa Ekaristi.

Mt. Eliji ni msimamizi wa masonara-wafua vyuma na dhahabu-Alikufa mwaka 660, tarehe 1 Desemba.

Maoni


Ingia utoe maoni