Jumanne. 07 Mei. 2024

Mt. Mwenyeheri Anwarite (Mtawa Na Mfiadini)

Mwenyeheri Anwarite (Mtawa Na Mfiadini)

Alfonsina Nengepeta alizaliwa mjini Wamba (Zaire) mwaka 1939 akiwa mtoto wa nne wa Amisi Badjulu na Juliana Isude. Alipofikia umri wa kutosha, alienda kusoma shuleni, na siku ya kwanza alipelekwa na mkubwa wake ambaye alikuwa aKiitwa jina lake Leontina Anwarite. Badala ya kuandika Alfonsina Nengepeta', Hivyo akaanza kuitwa kwa jina la Anwarite.

Alipokuwa bado mtoto, alipenda sana kusali, na kila mara dada zake walipomzuia kusali kwa kumcheka na kumkejeli, alikasirika na kulia kwa sauti: "Sitaki kula bila kusali kwanza!" Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, alijiunga na chama cha watoto wa Ekaristi Takatifu. Alikuwa mfano na mwenye bidii na mwenye upendo kwa wanachama wenzake.

Mwaka 1955, alijiunga na shirika la masista wa familia Takatifu lililokuwa limeanzishwa katika mwaka 1936 huko Zaire. Akaanza kuitwa sista Maria Klementina. Siku moja baada ya kuweka nadhiri za kitawa, alishawishiwa sana na mama yake mzazi atoke utawani ili apate kusaidia shughuli za nyumbani. Lakini sista Anwarite akamjibu kwa ukali: "Wito ni kitu kikubwa. Hatuwezi kuuacha vivi hivi tu. Kwa hilo kosa lako, mama, utafanya malipizi kwa kusali Rosali nzima siku ya leo!"

Mwaka 1960, alihitimu masomo ya ualimu akapewa shahada. Ingawa alikuwa akikasirika haraka, kila wakati alipokuwa amechoka au kusikia maumivu ya kichwa, wanafunzi wenzake waliyaelewa mapendo yake. Alipokuwa katika hali ya kukasirika, alizoea kugugumia mithili ya bubu. Alipomkasirisha mwingine, yeye alinyamaa na kutulia kidogo ili afanye kila lililowezekana ili kumfurahisha yule aliyemkosea na kumwomba msamaha.

Mwaka 1964, nchi ya Zaire ilikuwa na balaa la mapinduzi. Watu walitishwa na habari za unyang'anyi na mauaji yaliyofanywa na askari waasi waliojaribu kuipindua serikali, nao walijiita simba. Mnamo tarehe 29 Novemba 1964, kundi la Simba lilifika kwenye konventi ya masista, nao wakaamriwa wajiandae kwa safari. Usiku walipumzika kidogo kwenye Misioni ya kijiji kimojawapo, na asubuhi safari ikaendelea tena. Mara kwa mara walilazimika kusikiliza kashfa za Askari. Walipowasili kijiji Isiro, masista walipelekwa kwenye nyumba mojawapo, lakini sista Anwarite na sista Kazima, aliyekuwa Mama Mkuu, waliamuriwa kubaki nyuma. Kanali Ngale akasema wazi kwamba anamtaka Sista Anwarite awe mke wake na kwamba usiku ule watalala pamoja. Mara akakemewa sana na Mama Mkuu akisema: "Jambo hilo halitawezekana kwa kuwa yeye ni bikira aliyebarikiwa kwa ajili ya Mungu". Kanali Ngalo akakasirika mno, akampiga Mama Mkuu kichwani na mikononi, naye akaanza kuvimba sehemu hizo; hata hivyo, hakuchoka kumtetea sista Anwarite. Basi, wakamchukua na kumpeleka kwenye chumba kingine, na Sista Anwarite akabaki yeye na askari tu. Nao wakamvua shela ya kitawa na kumpiga makofi.

Sista Anwarite akasema wazi: "Mimi sitaki kutenda dhambi hii. Iwapo unataka kuniua, basi niue". Alipopigwa kikatili na kanali Petro Olambe, akamwambia: "Nimekusamehe kwani hujui unalotenda". Wakati huo alikuwa ameangukia magoti, akapigwa tena kichwani na Kanali huyo huyo kwa kitako cha bunduki, akapoteza fahamu. Ofisa mwingine alipoingia katika chumba na kuitambua hasira kubwa ya Kanali Olombo, aliiondoa bunduki yake ili asije akawaua watawa wote. Lakini huyo aliposhindwa kuiona bunduki, akapiga mayowe na mara wakatokea vijana wawili wenye majambia. Wakaamriwa kumchoma Sista Anwarite. Basi, wakamrarua kinyama, kila mmoja wao akifanya hivyo mara nne au tano hivi. Kanali Olombo alipoipata tena bunduki, akampiga risasi Sista juu ya mkono wake wa kushoto, akatoka akawaita watawa wengine wauondoe mwili wake. Sista bado alikuwa akipumua, na ilikuwa wazi kuwa alikuwa katika hatua za mwisho ya kufa. Baada ya muda mfupi tu alikabidhi roho yake kwa Mungu. Ilikuwa mnamo tarehe 1 Desemba 1964. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na sita.

Licha ya Sista huyu kufundisha dhamani ya fadhila ya usafi wa moyo, lakini maishani mwake twaona vilevile ile bidii ya kuitawala hasira yake, pamoja na upendo mkubwa kwa Yesu wa Ekaristi na kwa Mama Maria. Alipokuwa anashawishiwa na kupigwa na askari, alikuwa na sanamu ndogo ya Mama Maria mfukoni. Waliitambua miezi sita baadaye walipoifukua maiti yake ili kuizika kwenye kaburi zuri na bora zaidi. Upendo wake kwao ulimwimarisha kuulinda usafi wa moyo. Papa alimtaja mwenyeheri mwaka 1986, wakati wa ziara ya kichungaji nchini Zaire.

Maoni


Ingia utoe maoni