Jumatatu. 06 Mei. 2024

Mt. Andrea, Mtume

Andrea, Mtume

Andrea, ndugu wa Simoni Petro, alizaliwa Betsaida mkoani Galilaya (Israeli), kwanza alikuwa mvuvi wa samaki, na mwanafunzi wa Yohani mbatizaji, halafu, alikuwa ndiye mtume wa kwanza aliyemfuata Bwana wetu. Siku moja alimsikia Yohani mbatizaji akisema juu ya Mwokozi: "Huyu ndiye mwanakondoo wa Mungu aondowaye dhambi za dunia"

Andrea alitafuta nafasi ya kuonana na Yesu. Yesu aliwauliza: "Mnatafuta nini?" Andrea na Yohane mtume walimjibu: "Mwalimu, unakaa wapi?" Hapo Yesu akawaambia: "Njooni, nanyi mtaona". Na hao wanafunzi wakamfuata Yesu, na kuona mahali alipokaa, na kushinda kwake siku ile.

Waliporudi, Andrea akamwendea Simoni nduguye akamwambia: "Tumemwona masiha aliyeaguliwa na manabii". Hata hivyo pengine aliendelea bado na kazi yake ya uvuvi kwa muda. Kwa sababu tunasoma katika Injili ya Marko kwamba Yesu alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliona wavuvi wawili, Simoni na ndugu yake Andrea, akawaambia: "Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu". Pale pale waliacha nyavu zao wakamfuata.

Hatusomi habari zaidi juu ya Andrea katika Injili, isipokuwa wakati Yesu alipowapa chakula watu elfu tano, na kumwuliza Filipo: " Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?, hapo Andrea alimleta mtoto kwa Yesu na kumwambia: "Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?

Mapokeo yanasema kwamba baada ya Pentekoste Andrea alihubiri injili katika sehemu mbalimbali, na kwamba hatimaye aliuawa msalabani huko Akaya (Ugiriki)

Maoni


Ingia utoe maoni