Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Katarina Laburee, Mtawa

Katarina Laburee, Mtawa

Wakatoliki wanaoifahamu medali ya Maria wa Mwujiza ni wengi, lakini asili ya medali hii hawaielewi. Ni Katarina Laburee aliyeagizwa na Bikira Maria katika Matokeo yake ili aitengeneze.

Akiwa na umri wa miaka ishirini na mitano, aliingia katika shirika la masista wa Vinsenti wa Paulo. Alikuwa msichana wa kawaida, mtulivu sana, baridi kidogo kitabia, na mwenye imani kubwa; aidha alimtegemea sana Bikira Maria, japo hakuidhihirisha kwa nje hiyo namna yake.

Akiwa bado mwanafunzi wa utawa, yaani kama mnovisi, alitokewa na Bikira Maria mnamo tarehe 27 Novemba 1820. Alimshirikisha tukio hilo kiongozi wake wa kiroho, naye aliandika hivi: "Mnovisi ameniambia kwamba wakati wa sala aliiona sanamu ya Bikira Maria kama vile kwenye picha, jinsi inavyooneshwa mara nyingi kwa jina la Mkingiwa dhambi ya asili; amesimama wima, ameinyoosha mikono na miale ikitoka mikononi mwake; maneno kama haya yalisikika: 'miale hii yaonesha neema anazozipata Maria kwa ajili ya binadamu; kando kando ya sanamu yalionekana maneno kama haya 'Maria uliyekingiwa dhambi ya asili, utuombee sisi tunaokukimbilia'. Baada ya dakika chache, sanamu ikageuka, na mnovisi aliona herufi 'M', juu yake aliona msalaba, na chini yake mioyo ya Yesu na Maria. Ndipo aliposikia tena sauti ikimwambia: ' Medali itengenezwe kadri ya mfano huo, na watu watakaoivaa medali hiyo iliyobarikiwa na kusali sala hiyo, watalindwa na Mama wa Mungu kwa namna ya pekee'.

Padre hakuyasadiki mara moja yote aliyoambiwa; akamshauri mnovisi kwamba njia yenyewe ya kumheshimu Maria na kulindwa naye ni kuishi kadri ya fadhila za Bikira Maria. Mnovisi Katarina akamwitikia kiongozi wake. Lakini miezi sita baadaye, alipata tokeo kama hilo hilo, na alipomwambia kiongozi wake, huyo akamshauri kama alivyofanya hapo kwanza. Baada ya nusu mwaka, tena mnovisi aliliona tukio hilo hilo kwa mara nyingine tena na kuyasikia maneno hayo hayo. Zaidi ya hayo, aliambiwa Maria hakuridhika kwa kuwa medali ilikuwa haijatengemaa bado. Basi, padre kiongozi alimwendea askofu naye akakubali medali itengenezwe na kusambazwa. Miezi kumi na minane baadaye, medali 150,000 zilikuwa zimekwisha tengenezwa tayari na kusambazwa.

Katika maisha ya Katarina, jambo la ajabu ni kuwa alikuwa mtu wa kawaida sana ambaye hakuyavutia macho ya watu. Utakatifu wake ulilingana na neno la 'Kumfuata Yesu Kristu' kwamba: 'Penda kutojulikana na kutoheshimiwa'. Aliishi utawani kwa muda wa miaka hamsini kama sista mwema aliyekuwa mfano kwa wengine, kwa upendo mkubwa alifanya kazi yake katika nyumba ya wazee na daima alikuwa tayari kumsaidia kila mmoja. Watu walioijua siri yake walikuwa wachache sana, nao waliilinda kama siri kuu. Sista Katarina alifariki tarehe 31 Desemba 1876. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1947, na sikukuu yake huadhimishwa tarehe 28 Novemba.

Maoni


Ingia utoe maoni