Jumatatu. 06 Mei. 2024

Mt. Leonardi wa Porto Maurisio, Padre

Leonardi wa Porto Maurisio, Padre

Padre huyo alizaliwa mjini Porto Maurisio (Italia) mwaka 1671, na jina lake lilikuwa Paulo Jeronimo Kasanova. Baba yake alikuwa na mashua, nayo aliitumia kupeleka shehena kati ya miji ya Porto Maurisio na Genoa. Paulo alipofika umri wa miaka kumi na miwili, alienda Roma kwa ajili ya masomo yake kwa vile alivyokuwa mtoto mwenye akili sana.

Miaka minne baadaye alitambua mvuto wa kuwa mtawa. Alisali sana apate kujua aingie shirika gani la kitawa. Siku moja, aliwaona mtaani mjinj Roma watawa wawili wakiwa wamevaa kimaskini na kuzama katika unyamafu. Akawafuata hadi monasteri walimoingia, akaomba akubaliwe kujiunga na shirika lao, nalo lilikuwa Shirika la Wafransisko. Akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili aliweka nadhiri zake za kitawa. Akaanza kuitwa Leonardi. Baada ya kujifunza falsafa na teolojia alipadirishwa.

Mara afya yake ilianza kumsumbua sana kiasi kwamba baada ya miaka mitano alimwahidi Bikira Maria kwamba, pindi atakapopona atajitolea katika kazi ya kuhubiri kwenye mafungo ya kiroho katika maparokia. Na ajabu, muda mfupi tu baadaye akawa na afya nzuri tena. Ndipo ilipoanza kazi yake yenyewe. Mwenyewe aliwahi kusema kwamba kazi ya kuhubiri katika mafungo ya kiroho haikumvutia, hata hivyo, aliifanya kwa bidii zake zote kwa muda wa miaka arobaini na minne.

Kipaji chake hasa kilikuwa lafudhi, yaani uwezo wa kuwasisimua watu kwa maneno yake. Chemchem ya uwezo huo, ilikuwa katika maisha yake mwenyewe ya kiroho: moto wa maisha yake matakatifu ndiyo uliyoyapa nguvu mahubiri yake. Daima alitembea kwa miguu toka parokia moja hadi nyingine, na kila mahali mahubiri yake katika mafungo ya kiroho, yaliandamana na mapinduzi ya kiroho. Wakosefu wengi sana walimrudia Mungu kutokana na mahubiri ya padre huyo mtakatifu. Ibada ya njia ya msalaba na ile ya kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu ndizo hasa alizowashauri watu wasishike, na hivyo, alieneza sana ibada hizo mbili.

Mwaka 1751 alienda mji wa Florensi (Italia ya Kaskazini), na mara hii, kwa sababu ya uchovu wake mwingi, hakusafiri kwa miguu bali kwa gari, kufuatana na amri ya Papa mwenyewe. Baada ya kuhubiri katika mji huo, njiani alipokuwa akirudi Roma, alaiugua sana. Mara alipoingia katika monasteri yake, alipewa sakramenti ya wagonjwa, akafa siku chache baadaye. Mnamo mwaka 1867 alitangazwa mtakatifu.

Mashauri ambayo Padre huyo Mtakatifu aliwapa wakristu wa siku zile, yaani kufanya mara nyingi ibada ya njia ya msalaba na pia ile ya kuheshimu Moyo Mtakatifu sa Yesu, yatufaa pia sisi wa siku hizo.

Maoni


Ingia utoe maoni