Jumanne. 07 Mei. 2024

Mt. Yohani Berkmans

Yohani Berkmans

Yohani alizaliwa katika kijiji cha Diest (Ubelgiji), mwaka 1599, katika familia ya watu wenye kumcha Mungu. Baba yake alifanya kazi ya kushona viatu, lakini kazi hiyo haikumpatia maslahi ya kutosha. Hivyo Yohani aliyetaka kuwa Padre, baada ya kujifunza Kilatini kwa muda wa miaka mitatu, aliambiwa arudi nyumbani. Baba alikuwa akihangaika sana kwa ajili ya kumtunza mke wake mgonjwa na watoto watano, kiasi kwamba, kwa maoni yake, kumwona Yohani dukani kulikuwa bora zaidi kuliko kumwona, akiwa kama Padre, kwenye altare. Lakini mwanae akamwambia: "Baba, nitaponea mizizi na maji tu mradi niruhisiwe kuendelea na masomo yangu". Babake akamruhusu, lakini fedha za matumizi yake yote zilikuwa juu yake kuzitafuta. Basi, akajipatia kazi nyumbani kwa padre mmoja na hivyo akaweza kujilipia ada ya shule.

Alipopata umri wa miaka kumi na sita, mapadre Mayesuiti walimpokea katika chuo chao mjini Meklin (Ubelgiji), na Yohani mara akawapita wanafunzi wenzake wote kwa elimu. Baada ya muda usio mrefu, aliomba ruhusa ya kuingia katika Shirika la Mayesuiti, nao wakamkubali. Juma moja kabla ya kuingia utawa aliwaandikia wazee wake: " Baba na mama, njooni kunitembelea niweze kuwaambia 'Karibuni' na 'Kwa herini', nanyi muweze kusema: "Tunamrudishia Mungu mwana wetu ambaye tulimpata kwa Mungu". Kisha kuingia katika shirika la Mayesuiti, Yohani alionekana kuwa na fadhila nyingi na aliifuata barabara kanuni ya Shirika. Nia yake kuu ilikuwa kuitenda kikamilifu kila kazi ya kawaida. Alivyoona yeye, si kazi iliyokuwa muhimu bali ile namna ya kuitenda kazi hiyo. Namna zake hizo hazikumfanya awe mkavu; la, hata kidogo; bali aliwapendeza wenzake kwa kicheko na utani wake, akapata jina la kupanga la 'Frater Hilaris', maana yake 'Ndugu Mchangamfu,

Baadaye, wakuu wake walimpeleka Roma (Italia) ili apate kujifunza falsafa. Chumba alimokaa huko kilikuwa ni kilekile alimofia Mt. Aloisi Gonzaga (tazama 21 Juni). Yohani aliufuata mfano wa mtangulizi wake katika kuuzingatia usafi wa moyo. Kabla ya Kupadirishwa, alipatwa na ugonjwa mkali sana. Hakuonesha dalili ya uchungu kufuatana na jambo hilo, bali alifurahi sana kuipokea Sakramenti ya wagonjwa. Aliwaomba mapadre waliomtunza wampe mikononi kitabu cha Katiba ya Shirika, rosali na msalaba wake. Hatimaye aliyataja kwa furaha majina ya Yesu na Maria, na palepale akafa mnamo mwaka 1621, akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili tu. Alitangazwa Mtakatifu mwaka 1888. Masalia yake yamo, pamoja na yale ya Mtakatifu Aloisi Gonzaga, katika kanisa la Mt. Inyasi mjini Roma.

Maoni


Ingia utoe maoni