Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Kolumbani wa Bobio (Abbati)

Kolumbani wa Bobio (Abbati)

Mt. Kolumbani alizaliwa Ireland mwaka 550 hivi. Alipoona duniani kumejaa hatari nyingi, alinuia kuingia utawa, lakini mama yake alimkataza. Kolumbani hakuridhika alipokataliwa na mama yake. Alikata shauri kuhama nyumbani kwao. Mama yake ili amzuie alijilaza chini kwenye kizingiti cha mlango. Kolumbani alikaza moyo akapita juu yake.

Kwanza alikwenda kusoma katika monasteri ya Bangor (Ireland), baadaye, alipata ruhusa kwenda kuhubiri Injili Ufaransa pamoja na watawa wenzake. Mfalme Sigeberti aliwapa jumba wakalifanya kama monasteri yao. Watawa hawa wakaanza kulima, na baada ya miaka michache nchi ilianza kustawi. Hapo zamani ilikuwa pori na mbuga tu, lakini watawa wake waliigeuza nchi ile ikawa mashamba mazuri.

Inasemekana kwamba siku moja Kolumbani alitaka kuingia katika pango lililochimbwa maweni, mara alimwona humo Dubu mwenye macho macho makali kama moto. Kolumbani asishtuke, alimwamuru Dubu kuondoka pangoni, naye dubu mara tu alikwenda zake kimya. Tukio hili ndilo asili ya Kolumbani kuonekana kwenye picha akiwa na dubu.

Kolumbani alijenga monasteri nyingi huko Ufaransa, ambazo aliziongoza kwa hali ya nidhamu iliyokuwa kali sana, ingawa hiyo, alipata wafuasi wengi. Kisha miaka kumi na miwili, yeye na watawa wa Ireland walifukuzwa kutoka Ufaransa. Basi, Kolumbani alikwenda Uswisi kueneza dini. Baadaye alimwacha Mt. Galli katika nchi ya Uswisi ayaongoze makabila ya huko katika dini ya Yesu Kristu. Mwenyewe alifunga safari kwenda Italia, huko akajenga monasteri ya Bobio. Kisha safari na kazi hizo zote, alienda kupumzika milele Mbinguni. Alikufa mwaka 615.

Maoni


Ingia utoe maoni