Jumanne. 03 Desemba. 2024

Mt. Klementi wa Kwanza

Klementi wa Kwanza

Mtakatifu Klementi aliongoka katika imani ya kweli kwa uongozi wa Mt. Petro. Katika barua zake Mt. Paulo (Fil. 4:3) alimtaja kama mwenzi wa masumbuko yake ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu kile cha uzima wa milele. Alikuwa Papa wa tatu baada ya Mt. Petro. Alilitawala Kanisa Katoliki kwa utaratibu na nguvu.

Inasemekana kwamba makafiri walimchongea kwa Kaisari Trayani, naye akamwamuru aitolee sadaka miungu ya Roma. Klementi alikataa katakata shauri hilo ovu, hiyo ndiyo sababu alikamatwa na kutumbukizwa kilindini mwa bahari akiwa na nanga shingoni kusudi apate kuzama ili wakristu wasiuzike mwili wake.

Mtakatifu Klementi aliwaandikia Wakristu wa Korinto (Ugiriki) barua yenye kusudio la kuwadumisha katika umoja na imani. Waliihifadhi barua hii ya kichungaji ili wapate mara kwa mara kuisoma katika makanisa yao.

Maoni


Ingia utoe maoni