Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Sesilia

Sesilia

Mambo yanayojulikana kwa hakika kabisa kuhusu Mt. Sesilia ni machache sana, nayo ni kwamba alikuwa bibi aliyekaa mjini Roma (Italia) karne ya tatu na kwamba alijitahidi kanisa lijengwe ambalo baadaye liliitwa 'kanisa la Sesilia'. Basi, ni hayo tu.

Sasa hadithi nzuri imetungwa juu ya maisha yake na jinsi alivyofia dini, nayo imeandikwa kwenye kitabu kiitwacho 'Mateso ya Mtakatifu Sesilia' ambacho kilimwonesha yeye kuwa mfiadini ambaye aliuawa kwa sababu ya upendo wake kwa Kristu. Sesilia alikuwa binti wa jamaa tukufu ya kiroma (Italia), aliingia ukristu na aliweka nadhiri ya ubikira ingawa wazazi wake walikuwa wapagani. Baba na mama yake walitaka kumwoza kwa nguvu kwa bwana mmoja jina lake Valeriani. Sesilia hakuweza kukimbia, alijiweka tayari kwa kufunga na kusali ili apate msaada wa Mungu katika masumbuko yake. Siku ya kuisheherekea harusi, watu wa nyumbani walipokuwa wakipiga zumari na ngoma, Sesilia aliimba rohoni mwake: "Ee Mungu wangu, uilinde roho na uulinde roho na uulinde mwili wangu safi, nisitiwe haya mbele za watu".

Usiku alipokutana kwa mara ya kwanza na mchumba wake, Sesilia alimwambia Valeriani: "Ninayo siri na sharti nikuambie. Karibu yangu husimama Malaika mkuu anayenilinda. Ukiniacha bikira atakupenda kama anavyonipenda mimi". Valeriani alishtuka, kisha akasema: "Nionyeshe basi Malaika huyo". Naye Sesilia alimwitikia: "Utamwona Ukibatizwa". Kwa shauri la Sesilia Valeriani alikwenda kumwomba Papa Urbano kufundishwa naye, kisha akabatizwa. Baada ya kubatizwa alirudi kwa Sesilia. Kumbe, mara alimwona malaika naye aking'aa kama jua akishikilia mkononi mataji mawili ya maua, akaliweka taji moja kichwani kwa Sesilia, na jingine kichwani kwa Valeriani.

Tibursi ndugu wa Valeriani aliposikia habari hii, akajisema kuwa naye ni mkristu. Wote wawili walikamatwa wakauawa. Liwali Almaki, aliwaza kwamba sasa ataweza kuwanyang'anya mali zao, lakini Sesilia akafanya haraka kuwagawia maskini fedha. Liwali alikasirika sana na kutaka kumshurutisha Sesilia kuzitolea sadaka sanamu za uwongo. Lakini Sesilia alijibu bila woga: "Afadhali nife kuliko kutoa sadaka kwa sanamu za mawe au chuma". Almaki akiogopa kwamba wangeanza kumfanyia fitina akatoa amri wampeleke Sesilia nyumbani kwake, wamfungie kwenye chumba cha mvuke kusudi wamzuie asipate kuvuta pumzi. Wakaitimiza amri hiyo, lakini Sesilia akawa bado yu hai. Mwisho liwali akamtuma mtesi kwenda kumkata kichwa kwa upanga chumbani. Mtesi huyo alimkata Sesilia kwa upanga mara tatu, lakini hakuweza kummaliza. Kwa kuwa ilikuwa imekatazwa kupiga zaidi ya mara tatu, akamwacha Sesilia pale pale amezimia. Alishinda siku tatu katika hali hiyo, akivumilia kufa kwa mateso makubwa hayo.

Mt. Sesilia husemwa kuwa yeye ndiye somo wa waimbaji wa kanisa kwa maana Sesilia aliimba rohoni mwake wakati wapiga musiki walipokuwa wakicheza zumari na kupiga ngoma katika sherehe ya harusi yake na Valeriani. Tunapomkumbuka leo katika Litirjia, tunamwendea Mungu kwa maombezi yake, na hasa tunawaombea wale wote ambao huwa wanajitahidi kufanya ibada za kanisa ziwe nzuri zaidi kwa musiki na nyimbo zao.

Maoni


Ingia utoe maoni