Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Andrea Avelino (Mtawa)

Andrea Avelino (Mtawa)

Andrea Avelini alizaliwa mwaka 1521 huko Napoli (Italia) akaitwa Lunseloti. Alipopewa Upadre kwanza alisomea sheria, kisha kuhitimu, alipewa kazi ya wakili katika kanisa, ndiyo kazi ya kukinga na kusimamia watu walioshtakiwa barazani. Siku moja alisema uwongo kidogo. Alipopata fahamu, alitubu kosa lake, akiondoka barazani asitake zaidi kuiponza roho yake, akaingia katika jamaa ya Wateatini, akachagua jina la Andrea kwa kuwa aliupenda sana msalaba na jinsi alivyouawa mtume Andrea. Aliweka nadhiri mbili: kwanza kutofanya alivyotaka mwenyewe, na pili kuendelea kila siku katika utakatifu. Ndiyo maana alijitesa kwa kudharau heshima na ukubwa.

Heshima ya Mungu ilimsaidia kuongoza roho za watu, na hasa wakati wa kuungamisha Mungu alimfumbulia siri zao. Alihubiri injili kwa watu wa mashamba karibu na Napoli kwa bidii kubwa. Moyo wa Ibada na uaminifu kwa katiba ya shirika lake vilikuwa sifa zilizomwonyesha kama mtu afaaye sana kwa kazi ya kuwalea wanovisi. (Maana yake wanafunzi) wa shirika lake la kitawa. Maaskofu wengi walizitambua sifa na vipaji vyake vingine, na waliutafuta sana msaada wake katika kuirekebisha hali ya majimboni mwao na maisha ya kikristu ya waumini wao. Mahubiri yake katika makanisa mjini Napoli yaliwaongoa wengi, na kuwa moto moto tena katika kuishi kadri ya imani yao.

Akiwa na umri wa miaka themanini na minane, siku moja alipoanza misa alipatwa na pigo la moyo asiweze kutamka neno. Walimpa sakramenti ya mpako wa wagonjwa, akafa siku hiyo hiyo mnamo mwaka 1608. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1712.

Maoni


Ingia utoe maoni