Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Hilda wa Witbi, Mtawa

Hilda wa Witbi, Mtawa

Mtakatifu huyo, Mwingereza, alibatizwa alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitatu, na aliishi maisha ya Kikristu na ya kifadhila muda wote kabla ya kuingia utawa. Alipofikia umri wa miaka thelathini na mitatu, aliamua kumtumikia Mungu utawani. Baada ya kukaa katika monasteri ndogo kwa muda usio mrefu sana, aliwekwa kuwa mama abati wa monasteri kubwa kidogo ambapo aliwaongoza wamonaki kuishi kwa nidhamu ya kiroho na kuwa moto moto katika utumishi wao wa Mungu.

Kadri ya desturi ya nyakati hizo, monasteri hiyo ilikuwa monasteri mbili tofauti, moja ya wamonaki na moja ya masista. Japo monasteri hizo mbili zilitengana kabisa, hata hivyo kanisa walimokuwa wakiimba sala rasmi ya liturjia ya Kanisa, lilikuwa moja tu, na mama abati alizisimamia monasteri zote mbili ila katika mambo yaliyohusu Sakramenti.

Mwaka 657 alianzisha upya monasteri kule Witbi (Uingereza). Chini ya uongozi wake, ikajulikana sana kwa ajili ya elimu na maktaba iliyojengwa huko. Pia mwenyewe aliwafundisha wamonaki na masista sarufi na fasihi ya lugha ya Kilatini, na wote walisukumwa naye kusoma sana Biblia. Walikuwapo watu wengi waliomwendea kuomba ushauri, sio tu wamonaki na masista, lakini pia wafalme, watawa na watu wa kawaida. Mtakatifu Hilda alipendwa sana na wote walioongozwa naye, hasa wakazi wa monasteri hizo mbili.

Miaka saba kabla ya kifo chake alipatwa na ugonjwa ambao polepole uliongezeka na kumdhoofisha. Utendaji wake wa kazi ulipungua, lakini kamwe haukuisha kabisa mpaka siku ya kufa kwake. Katika muda huo wote, licha ya hali mbaya ya afya yake, hakuacha kumshukuru Mungu Muumba wake, na kuwapa moyo masista na wamonaki wake wadumu kumtumikia Mungu kwa uaminifu, hata wakiwa dhaifu au wagonjwa. Alifariki dunia mnamo tarehe 17 Novemba mwaka 680.

Jambo la ajabu ni kwamba jina lake lilionekana katika kalenda ya liturjia aliyoitumia Mt. Wilibrodi, mwaka 710 hivi, yaani miaka thelathini hivi baada ya kufa kwake. Kwa hiyo, ni wazi kuwa upesi sana utakatifu wake ulitambuliwa kule Uingeteza, akaanza kuheshimiwa kama Mtakatifu. Kwa Mtakatifu Hilda twaona jinsi zamani zile mwanamke mwenye vipaji alivyoweza kufikia hadhi ya uwezo na mamlaka katika Kanisa.

Maoni


Ingia utoe maoni