Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Elizabeti wa Hungaria, Mtawa

Elizabeti wa Hungaria, Mtawa

Elizabeti binti wa mfalme wa Hungaria, alizaliwa mwaka 1207. Aliposwa na Lui wa Turingia (Ujerumani) alipokuwa mtoto bado. Alimzalia watoto watatu. Mumewe alimpenda sana, kwani Elizabeti alikuwa ni mwanamke bora, aliyefanya kila kitu ili kumpendeza mumewe. Kwa desturi ya wakati ule, wafalme na malkia walivaa kofia za dhahabu, lakini Mt. Elizabeti kila mara alipoingia kanisani aliivua kofia hiyo. Ni shida sana kusema ni jinsi gani alivyowapenda maskini. Aliwapa kila kitu alichokuwa nacho, na aliwagawia chakula kilichobaki. Wagonjwa na maskini wa nchi nzima walimwita mama yao. Wakoma walikuwa wapenzi wake wakubwa.

Siku moja, mumewe alimkuta njiani, wakati wa baridi na dheluji, akisema: "Umechukua nini tena katika nguo yako?" Elizabeti mara aliifungua nguo yake, na mara lo! Mahali pa vyakula yalitoka mawaridi mazuri yenye harufu tamu ajabu.

Elizabeti na bwana wake na watoto wao walifurahi raha ya familia. Wote walipendana sana, lakini hatimaye alipatwa na uchungu mwingi. Kwanza mumewe alikwenda kupigana na Waislamu katika Nchi Takatifu, alikufa njiani. Alipopata habari hii, Elizabeti alikuwa na huzuni kubwa mno, akilia kwa sauti kubwa. Watu waliogopa kuwa angekua mwehu.

Halafu Henriko alimfukuza katika nchi, pamoja na watoto wake watatu. Lakini mwisho ndugu zake walimhurumia wakampa haki yake. Elizabeti aliwasamehe wale waliomtendea vibaya vile. Alishauriwa na wengi kuolewa tena, lakini akakataa kabisa. Badala yake aliamua kuishi kitawa, akajiunga na utawa wa tatu wa Mtakatifu Fransisko. Aliendelea kuwatunza wagonjwa na maskini, akizoea kwenda kuvua samaki ili awalishe, na kushona nguo awavike walio fukara.

Kiongozi wake wa roho, padre Konrad wa shirika la Mt. Dominiko, alikuwa mtu wa elimu na vipaji vingi, lakini huruma yake haikuwa nyingi, na hivyo alikuwa mgumu. Katika njia yake ya kumwongoza Elizabeti alikuwa mkali, pengine hata katili, na Elizabeti alikubali kabisa kwamba alimwogopa. Lakini hata hivyo alibaki mwaminifu, mnyenyekevu na mtii kwake. Mwenyewe alieleza kuwa alifanana na matawi: aliinama wakati wa dhoruba, kisha akajiinua tena bila kuvunjika. Kweli, uvumilivu wake mbele ya kiongozi huyo ulikuwa mkubwa ajabu. Hakuishi hivyo muda mrefu. Alifariki dunia mwaka 1231 akiwa na umri wa miaka ishirini na minne tu. Huenda mazoea yake makali ya kujikatalia, na uongozi mgumu mno, vilichangia kuyafupisha maisha yake. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1235.

Maoni


Ingia utoe maoni