Getruda wa Helfta
Getruda alizaliwa mwaka 1256 huko Eisleben (Ujerumani). Alipokuwa na umri wa miaka mitano, aliwekwa chini ya utunzaji wa watawa wa Sistersia huko Helfta. Kwa kuwa alikuwa ni mtoto mwenye akili nyingi, aliruhusiwa kujifunza Kilatini, falsafa, teolojia, mziki na kutengeneza picha za rangi. Alipopata umri wa miaka 20 Bwana wetu Yesu Kristu alimfumbulia mengi yasiyoandikwa vitabuni. Muda wa miaka mingi alimwona Yesu kila siku. Toka wakati ule alibadili namna yake ya kuishi; alizidi kusali akitumia sala za Liturjia, alisoma hasa Biblia na vitabu vya Mababu wa Kanisa, akaandika vitabu vya fikara na vya sala.
Alichukia majivuno, na alipendelea kuwaza rohoni mwake mapendo ya Yesu Kristu aliyetuponyesha kwa mateso yake na katika Sakramenti ya Ekaristi. Siku moja Bikira Maria alimtokea amevaa joho pana sana, na chini ya joho hilo walijificha wanyama wakali wengi. Mama wa Mungu aliwabembeleza wanyama wale na wakawa wapole kama kondoo. Ndivyo Bikira Maria alivyotaka kujionyesha kama yu makimbilio ya wakosefu.
Gertruda alitamani jina la Mungu lisifiwe na watu wote. Kwa sala na mateso na mazungumzo yake, alifanya bidii kuwaongoza wakosefu. Hakusahau pia roho za marehemu zinazoteswa toharani; na Bwana wetu alimfumbulia jinsi wanavyoteswa kwa mateso makali. Gertruda alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka kumi. Alikufa mwaka 1301, alipokuwa na umri wa miaka 45.
Maoni
Ingia utoe maoni