Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Margareta (Malkia wa Skotilandi)

Margareta (Malkia wa Skotilandi)

Margareta alizaliwa mwaka 1046, akawa mjukuu wa mfalme Edmund wa Uingereza. William wa Normandia alipoiteka kwa nguvu nchi ya Uingereza, Edgardi kaka yake Margareta hakuweza kushindana naye. Basi, alijipakia Merikebuni kwa siri, pamoja na dada yake Margareta. Walikokotwa na mawimbi ya bahari kwa muda wa siku nyingi, mpaka wakafika Pwani ya Skotland.

Mfalme wa huko, Malkolm wa Tatu, aliwapokea vizuri nyumbani kwake, naye mfalme alipendezwa sana na uzuri wa Margareta na utakatifu wake, hivyo alitamani kumwoa. Margareta alikubali, mwaka 1370, akamzalia mfalme Malkolm watoto wanane, wanaume sita na wa kike wawili. Katika siku za maisha yao walisaidiana kutawala nchi, na ilistawi sana, kwa maana raia walimpenda Margareta kama mam yao. Kazi yake ilikuwa kuwatuliza wenye uchungu, kuwatunza maskini na kuwalisha yatima.

Mfalme Malkolm alikuwa hana mwenendo wa kupendeza, adabu zake zilikuwa haba na alikasirika upesi; lakini nia yake ilikuwa nzuri. Kwa kuwa alitambua kwamba Kristu alikaa moyoni mwa Malkia wake, kwa hiyo alikuwa radhi kuyafuata mashauri yake. Hivyo Malkia Margareta aliweza kumwongoza Malkolm, kuilainisha tabia yake ngumu, na kumfanya awe mfalme mwenye fadhila nyingi: upendo wa kidugu, haki na huruma.

Huenda fadhila kuu ya malkia huyo ilikuwa upendo wake kwa maskini. Mara nyingi aliwatembelea wagonjwa, na hata aliwauguza mwenyewe. Hasa wakati wa Majilio na Kwaresima yeye na mfalme waliwalisha maskini mia tatu vyakula vile vile walivyokuwa wakila wao wenyewe. Mtakatifu Margareta alitumia kila siku saa fulani kwa sala na kuitafakari injili.

Mwaka 1093, siku nne kisha kupata habari kwamba mume wake Malkolm alikufa katika vita, Margareta alifariki huko Edinburgh, akiwa na umri wa miaka arobaini na saba. Alitajwa kuwa mtakatifu mwaka 1250. Mtoto wake Daudi, aliyekuwa baadaye mfalme wa Skotland anatukuzwa pia kama mtakatifu na watu wa Skotland.

Maoni


Ingia utoe maoni