Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Didas wa Sevila

Didas wa Sevila

Didas alizaliwa na wazazi maskini sana nchini Hispania mwaka 1400. Alitaka kujiunga na Padre Mtakatifu aliyeishi upweke, na baada ya kumwomba mara nyingi, mwishowe, alimkubali. Kijana alisali sala zote alizozisali padre huyo, na mazoea yake ya kufanya kitubio nayo aliyafanya yote. Kazi yao ya pamoja ilikuwa kulima bustani ya mboga na visahani, umma na vijiko vya miti.

Baada ya miaka kadhaa alirudi nyumbani, lakini hakukaa sana. Akaingia utawa wa Mt. Fransisko, akawa Bruda katika shirika lao. Baada ya kuweka nadhiri za utawa alitumwa kama mmisionari kufanya kazi katika visiwa vya Kanari, vilivyo karibu na mwambao wa Afrika ya kaskazini-magharibi. Hapa alichapa kazi sana, hasa ile ya kuwafundisha watu dini na kuwaongoa. Twaambiwa kwamba katika nyumba yao ya kitawa alikuwa akitafuta kazi zile zilizokuwa duni. Aliheshimiwa sana, kwa moyo wake wa sala, bidii zake katika kutekeleza wajibu wake, na unyamavu wake, maadili hayo yaliwashangaza wote waliomfahamu. Ndiyo sababu mwaka 1445, ingawa alikuwa Bruda, aliwekwa kuwa mkuu wa nyumba. Miaka minne baadaye, alihamishwa na kurudi Hispania.

Mwaka 450 watawa Wafransisko wengi walisafiri kwenda Roma (Italia) kwa ajili ya adhimisho la jubilee fulani, na pia kwa ajili ya kushiriki Ibada kuu ya Padre Bernardini wa Siena wa shirika lao kutangazaa Mtakatifu (taz. 20 Mei). Bruda Didas naye alipewa nafasi ya kwenda. Wakati ule, ugonjwa wa tauni ulianza kuenea mjini Roma, na kwa bahati mbaya uliwaambukiza wengi wa watawa wenzake. Bruda Didas alijitolea kwa moyo wake wote kuwauguza, na kama si kwa ajili ya bidii zake, hakika, wengine wangalikufa. Inasemekana kwamba wengine aliwarudishia afya kimiujiza kwa sala zake. Hivyo ndivyo alivyoshughulika kwa muda wa miezi mitatu.

Alirudi Hispania, ambapo aliendelea kuishi kwa muda wa miaka kumi na mitatu. Mwaka 1463 aliugua sana, akafa akiwa na msalaba mkononi akidondoa maneno ya Lutrujia ya Ijumaa Kuu ya Siku zile: "Mti bora, misumari bora, wachukua uzito ulio bora". Bruda Didas alitangazwa kuwa mtakatifu mwaka 1588.

Maoni


Ingia utoe maoni