Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Stanislausi Kostka

Stanislausi Kostka

Stanislausi Kostka ni mfano mzuri sana wa vijana Wakristu. Alizaliwa Poland mwaka 1550, na wazazi wa jamaa bora. Kuhusu tabia yake, alitofautiana sana na mkubwa wake Paulo. Hata katika utoto wake Stanislausi alikuwa mzito, ambaye alitumia muda mrefu kusoma na kusali; Paulo alikuwa mchangamfu aliyeipenda michezo na maongezi, hakusali sana na alikuwa akimwangalia mdogo wake kuwa ni mtakatifu mno. Baadaye, wote wawili walienda Vienna (Austria) wapate kujifunza kwa Mayesuiti. Mlezi wao aliwapangisha katika nyumba ya Mprotestanti, na Stanislausi alisumbuliwa sana na mtu huyo. Hata nduguye Paulo alitaka kumpoteza kwa anasa za dunia. Lakini Stanislausi alikaa imara. Kila siku alikuwa akishiriki Misa na kupokea Kumunyo takatifu. Alimwita Bikira Maria mama yake, na hakukosa kusali Rosali.

Kwa mwenendo huo Stanislausi, alimpendeza kila mmoja na kumvutia kwake, lakini hali hiyo haikumfurahisha Paulo hata kidogo. Kwa hiyo, alianza kumkejeli mdogo wake na kuzidhihaki sala zake na ule moyo wake wa ibada. Hivyo, Stanislausi akaanza kujisikia vibaya na kukosa raha, hata akashawishika kutoroka. Lakini hakufanya hivyo; badala yake, alishikilia zaidi kanuni zake, akibaki mwaminifu kwa sala, misa na komunyo. Na kadri Stanislausi alivyozidi kuwa mwaminifu, vivyo hivyo ndivyo alivyozidi kuchukiwa na Paulo.

Baada ya miaka miwili, Stanislausi akawa mgonjwa sana, akataka kupokea Kumunyo kitandani mwake. Mwenye nyumba Mprotestanti alikataa kabisa Ekaristi Takatifu kupelekwa ndani ya nyumba yake. Stanislausi alimwomba Mtakatifu Barnaba kumsaidia katika shida yake. Inasemekana kwamba Bikira Maria alimtokea pamoja na Mtoto Yesu Mikononi, akamwambia kifo chake kilikuwa bado, kwanza amtukuze Mungu katika Shirika la Mayesuiti.

Lakini mkuu wa Mayesuiti huko Vienna ( Austria) hakuthubutu kumpokea kwa sababu aliogopa baba yake Stanislausi atakasirika sana. Basi, Stanislausi akaamua kwenda Roma kuomba ruhusa kwa mkuu wa shirika zima. Kwanza alienda kuonana na mkuu wa Mayesuiti wa Ujerumani, naye alivutwa na kijana huyo kwa ajili ya mwenendo wake na namna zake zilizoonyesha unyenyekevu na heshima. Basi, akamruhusu kwenda Roma ambapo, mwaka 1567, mkuu wa Shirika ambaye siku zile alikuwa Mt. Fransisko Borjia (taz. 10 Octoba), alimpokea shirikani. Baba yake alipopata habari hii, alikasirika sana kwa sababu-alivyosema-"Kijana huyu aliifuatia njia isiyolingana hata kidogo na asili yake bora sana". Kwa heshima kubwa Stanislausi alimwandikia barua baba yake kwamba hawezi kuukubali uamuzi wake.

Stanislausi alikuwa na umri wa miaka 17, akawatangulia wanafunzi wenzake kwa utii na ibada. Moyoni mwake yaliwaka mapendo ya Mungu. Walipotaja jina la Maria alishtuka kwa furaha. Kwake Stanislausi amri ya padre ilikuwa kama amri ya Mungu mwenyewe. Muda mfupi tu baada ya kuingia shirika na kuanza malezi ya kiroho katika novisiti, aliugua sana akafa mwaka 1568. Alipozimia alisikika akisema: "Namwona Bikira Maria na kundi la Malaika, wakija kuipokea roho yangu".

Mwezi mmoja baadaye alifika mdogo wake Paulo ili, kwa niaba ya baba yake, kumwamuru Stanislausi arudi nyumbani. Alishtuka mno, alipoambiwa ndugu yake amefariki dunia. Akahuzunika kupita kiasi, hasa kwa ajili ya vile alivyomtendea mdogo wake mara nyingi na kwa muda mrefu. Tangu saa hiyo, Paulo huyo aliibadili kabisa namna yake ya kuishi. Stanislausi alitajwa kuwa Mtakatifi mwaka 1726.

Maoni


Ingia utoe maoni