Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Yosafati wa Polotski

Yosafati wa Polotski

Mt. Yosafati alazaliwa huko Ukraine (Urusi), mwaka 1580. Wazazi wake walikuwa Wakristu hodari wa Kiortodoksi wenye cheo na heshima. Akiwa angali kijana aligeuka kuwa Mkatoliki. Akaingia katika Utawa wa Mt. Basili, akawa mfano wa kila fadhila. Akateuliwa kuwa abati wa Monasteri yake na baadaye askofu mkuu wa Polotski, katika nchi ya Poland. Akiwa na cheo hiki hasa alishughulika kuziunganisha pande mbili za kanisa, yaani upande wa Kilatini na upande wa Kigiriki, ambao ulijitenga na enzi ya Papa wa Roma.

Askofu Yosafati aliwasaidia Wakristu wengi wa Kiortodoksi, hasa wale walioishi katika jimbo lake, kugeuka kuwa wakatoliki na kumtii tena Papa wa Roma. Wale walioongoka hivyo, hawakulazimika kubadili kanuni zao za kufanya ibada. Hilo lilikuwa jambo kuu sana wakati ule. Wakristo wa Kiortodoksi hutumia lugha ya Kigiriki na kufuata mila za mashariki. Kwa uamuzi wa askofu Yosafati, Waortodoksi waongoka waliruhusiwa kuendelea na kawaida hiyo, badala ya kuanza kutumia lugha ya Kilatini na kushika mila za nchi za Ulaya ya Magharibi kama walivyofanya wakatoliki wengine wote. Katika suala hilo lote askofu Yosafati alitaka kuona tena umoja wa Kanisa, yaani wote nyuma ya Papa wa Roma; na machoni pake jambo la lugha na mila lilikuwa dogo tu. Lakini kwa Wakuu wengine wa dini, hilo lilikuwa jambo kuu sana, na hivyo bidii za askofu Yosafati hazikuthaminiwa kila mahali.

Kwanza, askofu wa Kiortodoksi wa Polotski alianza kufanya fujo dhidi ya Yosafati, na hata kumsingizia uwongo alipotambua kwamba Waortodoksi wengi wamekuwa Wakatoliki. Kwa kuwa kila askofu alikuwa na watu wenye kumuunga mkono, fujo kubwa ikatokea. Hali hiyo ikawa mbaya zaidi kwa vile maaskofu Wakatoliki wa nchi ya Poland hawakumwunga mkono askofu mwenzao. Badala yake walimlaumu na kumkasirikia kwa sababu hakuwalazimisha waongoka wale kutumia lugha ya Kilatini na kushika mila za Magharibi.

Siku moja askofu Yosafati alipokuwa safarini akikagua makanisa yake, kundi kubwa la Waortodoksi lilitaka kumwua. Basi, akawaambia: "Mimi nipo hapa kama mchungaji wenu. Mjue kwamba kwa furaha natoa uhai wangu kwa faida yenu na kwa ajili ya umoja mtakatifu wa Kanisa". Basi, wakamwacha.

Lakini siku nyingine tena, mnamo tarehe 12 Novemba mwaka 1623, wengine walitaka kuishambulia nyumba yake. Walipoanza kuwatendea watumishi wake kwa udhalimu, Yosafati akawatokea akawaambia: "Mkiwa na shida nami, mimi nipo hapa. Msiwasumbue watu wengine". Mara walimrukia, wakampiga makofi na ngumi, wakamchoma mikuki na visu, mwisho walimpiga kwa upanga, wakamtupa mtoni. Damu yake iliwanufaisha wauaji wake wa kwanza, kwa kuwa walipohukumiwa kufa, walijuta dhambi yao ya ufitini, wakawa wakatoliki. Mt. Yosafati alikufa mfiadini mnamo mwaka 1623. Alitajwa matakatifu mwaka 1867.

Maoni


Ingia utoe maoni