Martini wa Tur
Martin alizaliwa mwaka 316 katika mkoa wa Panonia (Hungaria) katika familia isiyo ya kikristu. Mzee wake alikuwa Ofisa katika jeshi la Roma, na Martin alimfuata: alikuwa mwanajeshi akiwa na umri wa miaka kumi na mitano. Miaka mitano kabla hajaingia jeshini aliwahi kujiandikisha kuwa mwanafunzi wa dini, lakini wazee walimzuia asibatizwe. Mwenendo wake huko jeshini ulielekea zaidi kwa ule wa mtawa kuliko wa askari kwa vile alivyokuwa mwema na mpole.
Mfuasi wake Sulpisi Severi ndiye aliyeandika hadithi ya yule maskini aliyemwomba chochote. Tufanyeje? Martin alimwona uchi, mwenye hali mbaya, akitetemeka kwa baridi na njaa. Martin hakuwa na chochote ila panga na joho lake. Basi, kwa panga lake alilikata joho lake, akampa nusu yake yule maskini. Usiku ule Bwana Yesu, hali amevaa nusu hiyo, alimtokea katila ndoto, akisema: "Martin mkatekumeni ndiye aliyenivika vazi hili". Baada ya ndoto hiyo, Martin alijitafutia nafasi ya kubatizwa upesi.
Miaka michache tu baadaye akiwa na umri wa miaka ishirini, alilotoka jeshi kwa sababu kama alivyosema mwenyewe: "Mimi ni askari wa Yesu. Si halali kwangu kupigana vita". Ili kumtumikia Mungu faraghani, alijiweka chini ya ulinzi wa askofu Hilary wa Pwatye (Poitiers, Ufaransa, taz. 13 Januari). Askofu huyo alimpa shamba ajijengee nyumba ndogo aweze kukaa upweke, lakini haraka sana wengine, wenye nia kama hiyo ya kukaa upweke, walitaka kujiunga naye. Hivyo Martin alijenga Monasteri. Aliishi hapa kwa muda wa miaka kumi, na wakati huo alipadirishwa, akaanza kujulikana sana kwa ajili ya mahubiri na miujiza yake.
Alipokufa askofu wa Tur (Tours, Ufaransa), wakristu wa huko walitaka Martini ashike nafasi yake, lakini Martin hakutaka. Basi, watu waliamua kumnasa. Aliitwa kwenda mjini kumhudumia mgonjwa, na mara baada ya kumsaidia wakristu wakaja, wakamchukua na kumpeleka kanisani ambamo maaskofu wengine walikuwepo kwa ajili ya uchaguzi. Hao hawakumwona Martin anafaa, lakini mapadre na waumini walisisitiza. Basi, Martin akawa askofu wa Tur.
Alisafiri katika jimbo lake akihubiri injili kila mahali; alizibomoa hekalu za miungu wa uongo, aliwinga mashetani na alitenda pia miujiza mingi. Alikuwa na huruma kwa watu wote, na mara nyingi aliwaombea msamaha wale waliohukumiwa kufa. Hivyo utawala wa Bwana Yesu ulizidi kuenea. Aliitangazia tarehe hasa ya kufa kwake. Akiwa safarini katika jimbo lake aliugua, na muda usio mrefu baadaye, akafa, mwaka 397. Alikuwa na umri wa miaka themanini. Fundisho kuu tunalolipata katika maisha yake ni wazi sana, nalo ni upendo wa kidugu kufuatana na maneno ya Yesu: "Kadri unavyomtendea mmojawapo wa wadogo zangu, umenitendea mimi; nilikuwa uchi, nanyi mkanivika.
Maoni
Ingia utoe maoni