Jumapili. 05 Mei. 2024

Mt. Leo Mkuu

Leo Mkuu

Alizaliwa Italia, lakini haijulikani ni kwenye sehemu gani wala hakuna habari yoyote juu ya miaka ya ujana wake. Anajulikana kwanza kama Shemasi na msaidizi wa Papa. Kwa Shemasi kumasaidia Papa katika mambo ya maana sana, ilikuwa kawaida ya siku zile. Mwaka 440 alitumwa Ufaransa kwa majemedari wawili wa majeshi ya Roma yaliyokuwa yakikaa Ufaransa. Majemedari hao walikuwa wanagombana sana na ugomvi wao uliihatarisha sehemu kubwa ya milki ya Roma kushambuliwa na watu wa makabila mengine, na hata kutwaliwa nao. Shemasi leo alifanikiwa kuwapatanisha.

Alipokuwa anautekekeza bado ujumbe huo, Papa Sisto alifariki dunia, na Shemasi Leo alichaguliwa kushika nafasi yake, mnamo mwaka 440. Tangu hapo alipata nafasi nyingi zaidi za kutumia vipaji vyake vingi sana. Alijitokeza kama mtaalamu wa teolojia na mchungaji hodari, pia kama mtawala mwenye busara wa nchi na mwenye uwezo katika menejimenti ya mali ya Kanisa. Kwa ajili ya shughuli zake kuu alizofanya katika maeoneo kadhaa alijistahilisha sifa ya 'Mkuu'

Alimwandikia barua Kaisari Teodosio ambaye kuyaingilia katika mambo ya Kanisa, alisababisha fujo kati ya baadhi ya maaskofu. Alimwarifu hivi: "Uwaachie maaskofu uhuru wa kutetea imani kwa kuwa hakuna uwezo wa serikali utakaofaulu kuiangamiza".

Kuhusu matukio ya kisiasa ya siku zile, Papa Leo alikabiliana na mambo makuu kweli. Atila, Mfalme wa kabila la Wahuni, na Genseriki, Mfalme wa Kabila wa Wavandali, wote wawili pamoja na majeshi yao, walielekea upande wa kusini; kila nchi waliyoipita katikati yake, iliangamizwa kabisa nao. Hofu kubwa ilienea kila upande, hasa walipoanza kuuelekea mji wa Roma. Papa Leo aliwaendea Wafalme hao wawili, akafaulu kuafikiana nao kwa kiasi. Hao waliahidi kwamba watawazuia askari wao wasiwaue watu wala kuchoma moto nyumba yoyote. Basi, askari wao waliivamia Roma, wakajirizisha sana, na majuma mawili baadaye, wakatoka wenye mateka wengi na mali nyingi sana.

Jambo kuu kabisa ambalo Kanisa linawiwa naye, ni mafunzo yake wazi sana juu ya Yesu Kristu kuwa na nafsi moja, yaani ile ya kimungu, na hali mbili, nazo ni ya kimungu na ya kibinadamu. Toka Roma aliwaandikia barua maaskofu waliokuwepo kwenye mtaguso mkuu mjini Kalsedoni (Uturuki) mwaka 451, juu ya suala hilo, naye ilikuwa wazi hata jumuiya yote ya maaskofu wakasema kwa pamoja: "Petro amesema kwa njia ya Leo". Tangu siku ile ufafanuzi wake Papa Leo umekuwa maelezo rasmi ya Kanisa.

Tumaini lake kwa Mungu lilikuwa kubwa kwa kila hali, haidhuru iwe mbaya kiasi gani; na kwa hiyo, hakuweza kamwe kukata tamaa. Kipindi chake cha upapa kilidumu muda wa miaka ishirini na mmoja; wakati huu aliupata upendo wa kila mmoja, wa matajiri na maskini, wa makaisari, mapadre na waumini wote. Alifariki dunia mnamo tarehe 10 Novemba mwaka 461, na masalia yake yamehifadhiwa kwenye basilika la Vatikano.

Maoni


Ingia utoe maoni