Kutabarukiwa Kanisa Kuu La Laterani
Hapo awali neno 'Letarani' lilikuwa jina la ukoo wa watu matajiri walioishi mjini Roma kwemye jumba kubwa sana. Mwaka 310, Papa alipewa jumba hili kama zawadi na Kaisari wa Roma aliyeongoka kuwa Mkristu. Papa huyu akalifanya kuwa ikulu yake, na jina 'Laterani' liliendelea kulitambulisha jumba hilo; baadaye, liliendelea kuwa jina la kanisa lililojengwa karibu na makao makuu hayo ya Papa, nalo likawa kanisa kuu la askofu wa jimbo la Roma, ambaye ni Papa wa kanisa zima. Neno 'basilika' ni jina la heshima ambalo makanisa mengine yamejaliwa kupewa na Papa kufuatana na ukuu wao.
Sikukuu ya leo hukumbuka kuwekwa wakfu kwa kanisa hilo ambalo kwa vile ni kanisa kuu la Papa, ni kama kanisa kuu la dunia yote. Maneno ' mama na kichwa cha makanisa yote ya mjini na ya ulimwengu' yameandikaa kwa lugha ya Kilatini kwa herufi kubwa sana kwenye ukuta wa mbele juu ya malango yake. Tunapoiadhimisha leo sikukuu hii katika Liturujia, twaudhihirisha umoja wetu wa jimbo la Roma, aidha upendo wetu kwa Papa aliye askofu wake.Basilika hili lilibarikiwa rasmi mnamo tarehe 9 Novemba mwaka 324 na Papa Mt. Silvester (taz. 31 Desemba), na akaliweka chini ya Kristu Mkombozi. Tangu basilika hili kujengwa, miaka mingi imepita, yaani miaka kama elfu moja mia sita. Basi, wakati wa muda huo mrefu basilika limestahimili matetemeko ya nchi, lilichomwa moto na kuumbuliwa vitani, lakini kila mara lilitengenezwa tena. Katika karne ya kumi na saba matengenezo makubwa yalifanywa na mafundi na wasanii ambayo yaliibadili kabisa sura ya basilika hili. Ndiyo sura yake wanayoiona watu siku hizi. Yasemekana ya kwamba ndani ya Altare kuu meza ya mbao imehifadhiwa ile ile aliyokuwa akiitumia Mt. Petro mtume kama altare.
Tunapokumbuka kuwekwa wakfu kwa basilika hili, tukumbuke kuwa haidhuru jengo liwe zuri namna gani, heshima yenyewe ya kila basilika, kila kanisa na kikanisa kinatokana na ukweli kwamba ni nyumba ya Mungu. Hiyo ndiyo sababu ya kuliheshimu kanisa la Parokia na Kigango na kulitunza katika hali ya usafi.
Maoni
Ingia utoe maoni