Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Francis wa Assisi

Francis wa Assisi

Mtakatifu Francis wa Assisi, alizaliwa mwaka 1182 huko Assisi, Italia. Baba yake aliitwa Pietro di Bernardone na mama Pica de Bourlemont. Alizaliwa wakati baba yake akiwa safarini Ufaransa, kibiashara.

Mtakatifu Francis wa Assisi jina lake la ubatizo ni Giovanni di Pietro di Bernardone. Lakini baba yake aliporudi alianza kumuita Francesco.
Mtakatifu Francis alisoma na kujifunza kilatini na muziki, na baba yake akamfundisha kifaransa na biashara, akitaka aje kurithi kazi hiyo.
Hivyo katika maisha ya ujana, mtakatifu Francis alifanya kazi katika duka la Baba yake.  
Mwezi Novemba, mwaka 1202 alienda vitani, ambako mtawala wa Assisi aliingia vitani na mtawala wa Perugia. 

Huko vitani walishindwa vibaya na wengi kuuwawa. Mtakatifu Francis, alichukuliwa mateka katika mji wa Collestrada na kukaa kwa muda wa mwaka mmoja.

Baada ya kuachiwa, alirudi katika maisha ya ujana ya kawaida. Lakini mwaka 1204 alipata maradhi yaliyomfanya kufikiria kuhusu aina ya maisha mengine, maisha ya kumcha Mungu.

Mwaka 1206 alienda hija katika mji wa Roma. Huko aliamua kubadili mavazi na kuwa ombaomba. Mtakatifu Francis, aliporudi, alitumia muda mwingi akiwa peke yake, hivyo akaenda kukaa nje ya mji katika pango dogo. Huko alipata maono ya kukarabati kanisa la San Damiano. 

Mtakatifu Francis akarudi nyumbani akachukua farasi wake pamoja na nguo zake, akaziuza, pesa akazipeleka kwa Padre wa kanisa hilo na kumuomba alikarabati. 

Baba yake alichukizwa na jambo hilo, akamfungia chumbani, kwa kuhofia kuwa , mwanae amepata tatizo la akili.
Baba yake aliposafiri, mama yake alimfungulia na kuwa huru. Baba yake aliporudi, alimtishia kuwa hatorithi kitu katika mali zake.

Tarehe 12 Aprili 1207, mtakatifu Francis alikutana na baba yake, mbele ya askofu Guido . Mtakatifu Francis alimwambia baba yake kuwa haitaji mali yake na anataka kufuata njia yake. Akamwambia kuwa anataka kumtumikia Mungu tu.

Hivyo akaondoka Assisi,  akaenda kuishi Gubbio, ambako alimkamata mbwa mwitu, aliyetishia maisha ya wakazi, na kumfuga.

Mwezi Februari tarehe 24, Mwaka 1209, Mtakatifu Francis alianzisha shirika la Wa Franciscan  na mwaka 1210, mwezi Julai, wakakubaliwa na Papa Innocent III, kuwa shirika, lakini hawakupata idhini kimaandishi mpaka mwaka 1223 mwezi Novemba tarehe 29,  kutoka kwa Papa Onorio III.

Katika kipindi cha uhai wake, miujiza mingi ilitendeka kwa kupitia mikono yake, akijenga nyumba na vituo vya wa Franciscan, alisafiri sehemu mbalimbali kuhubiri na kufundisha. Mtakatifu Francis alipata pia daraja la ushemasi,  alikufa mwaka 1226 October 3, katika kanisa dogo la Porziuncula katika mji wa Assisi, Umbria, Italia.

Alitangazwa mtakatifu mwaka 1228 Julai 16 na Papa Gregory IX alimtangaza kuwa mtakatifu tarehe 16 Julai, 1228.

Maoni


Ingia utoe maoni