Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Wilibrodi (Askofu na Mtawa)

Wilibrodi (Askofu na Mtawa)

Wilibrodi, mtume wa Uholanzi, alizaliwa Uingereza mwaka 658. Alipokuwa na umri wa miaka saba, wazazi wake walimpeleka shuleni katika monasteri, ili akasomeshwe. Toka hapo aliingia utawani, na kwa uongozi wa walimu wenye akili aliendelea katika maarifa ya dini kadhalika na katika maarifa mengine. Alipokuwa na umri wa miaka thelathini, alipadirishwa, akavuka bahari kwenda kuhubiri injili Uholanzi.

Alijaliwa kuwaongoa watu wengi wakawa wakristu katika dini katoliki, akajenga kanisa mjini Utrekt. Baadaye, alisafiri Roma, na huko alipata uaskofu kwa mikono ya Papa. Akarudi Utrekt, ambapo alijenga kanisa. Baadaye, akaanzisha monasteri mjini Echternach (Luksemburg), ambayo yakawa ni makao yake na kitovu cha utendaji wa shughuli zake. Toka hapa akaelekea tena kaskazini kuzieneza shughuli zake mkoani Friesland (Uholanzi). Akaenda kaskazini zaidi ili kuhubiri nchini Denmark, lakini hakufanikiwa.

Katika safari yake ya kurudi toka nchi hiyo, dhoruba ilimchukua, ikampeperusha hadi kisiwa cha Heligoland. Kwa maoni ya wakazi wake, kisiwa hiki kilikuwa mahali patakatifu, na kwa hiyo walidhani ni lazima kabisa kuulinda ukimya kila walapo, wanywapo kwenye chemchem au kuchinja mnyama. Wilibrodi akataka kuwasadikisha watu kwamba maoni yao yalikuwa potovu. Basi, akabatiza watu watatu kwenye chemchem yao, akachinja ng'ombe kwa ajili ya sikukuu. Muda wote alipokuwa anafanya hayo, alikuwa anazungumza kwa sauti. Wenyeji walikuwa na hakika kwamba Wilibrodi na wenzake watarukwa na akili, lakini wapi! Walipowaona kuwa ni wazima kabisa walikasirika sana na kujiuliza kama labda miungu wao walikuwa hawana nguvu tena; baadhi yao walisema kwamba miungu yao ilikuwa na uvumilivu mwingi sana. Mfalme alipoarifiwa juu ya matukio hayo, akaamuru mmisionari mmoja auawe. Basi, mmoja wa wandani wake Wilibrodi, akamfia Bwana Yesu.

Kutoka kisiwa cha Heligoland akarudi Uholanzi, akatelemkia kisiwa cha Walkeren. Hapo upendo na uvumilivu wake uliwavutia wengi kwenye dini ya kikristu, lakini Wilibrodi alipoiangusha sanamu iliyokuwa ikiangaliwa na wenyeji kama mungu wao, kasisi wake akakasirika sana na kujaribu kumwua Wilibrodi. Huyo akafaulu kujiokoa, akarudi salama Utrekt. Dini ya kikristo ilienea kwa taratibu katika sehemu nyingi za Uholanzi, mwenendo wa wenyeji wa mkoa wa Friesland ambao wakati ule walikuwa bado wakali na wakorofi, ulibadilika pole pole.

Mt. Wilibrodi alifariki dunia katika monasteri yake kule Echternach (Luksemburg), mnamo tarehe 7 Novemba 739. Alikuwa mzee mwenye umri wa miaka themanini na moja. Hati, aliyoiandika yeye mwenyewe, ipo bado imehifadhiwa mjini Paris (Ufaransa). Ndani ya hati hiyo aliandika kwamba alivuka Bahari ya Kaskazini mwaka 690, na kwamba aliwekwa wakfu kuwa askofu mjini Roma mwaka 695.

Maoni


Ingia utoe maoni