Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Zakaria na Elizabeti

Zakaria na Elizabeti

Zakaria na Elizabeti walikuwa wazazi wa Yohane Mbatizaji. Zakaria alikuwa kasisi wa agano la Kale, naye Elizabeti mkewe alikuwa wa jamaa ya Haruni. Wote walikuwa wacha Mungu. Walikuwa ni wenye haki mbele ya Mungu na waliendelea kuzishika amri zote za Bwana na maagazo yake bila lawama.

Walikuwa hawana mtoto maana Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana. Basi, Zakaria alipokuwa katika zamu akifanya kazi za ukuhani hekaluni, Malaika alimtokea akamwambia: "Usiogope Zakaria, maana dua yako imesikilizwa, na mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto mwanaume, na jina lake utamwita Yohane. Atakuwa mkuu mbele za Bwana; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye". (Lk. 1:5-15)

Mambo haya yakawa kama Malaika alivyosema. Elizabeti akamzalia Zakaria mtoto mwanaume, aliyeitwa Yohani, na sikukuu ya kuzaliwa kwake huadhimishwa 24 Juni. Baada ya kuzaliwa Yohani, hatukusikia habari zaidi za Zakaria na Elizabeti. Sikukuu yao inaadhimishwa sana katika makanisa ya Mashariki, na imeenea pia katika makanisa popote ulimwenguni.

Maoni


Ingia utoe maoni