Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Watakatifu Wote

Watakatifu Wote

Kanisa katoliki ni takatifu. Ni takatifu hasa kwa sababu kichwa chake, yaani Yesu, ni Mtakatifu, Mwana wa Mungu, Mungu nafsi ya pili. Aidha, Kanisa ni takatifu kwa sababu lilikuwa na watakatifu wengi tangu chimbuko lake, na litadumu kuwa nao mpaka mwisho wa dunia. Idadi yao ni kubwa sana, kiasi kwamba siku za mwaka hazitoshi kabisa kwa kuwaheshimu wote. Kuna mashahidi, mabikira na watakatifu wengine kwa maelfu, hata hatuwezi kuijua orodha kamili ya majina yao.

Kwa hivyo, Kanisa limeiweka sikukuu ya tarehe hii ya kwanza ya mwezi Novemba, ili iwe sikukuu ya kuwaheshimu hao wote. Na tena, Kanisa huwaambia watoto wake hivi: "Inueni mioyo yenu, matajiri kwa maskini, wakubwa kwa wadogo, wote kwa jumla tunahitaji heri na raha". Lakini raha hii ya milele, haipatikani hapa duniani. Hata hivyo, raha hii inaanzia hapa duniani kwa njia ya maisha safi katika Kristu. Roho zetu zitatulia tu ikiwa tutajaaliwa kumwona Mungu Mbinguni.

Watakatifu tunaowaheshimu hivi leo, walikuwa binadamu kama tulivyo sisi, walipigana vita dhidi ya tamaa za mwili, majivuno, mali, anasa, uzembe, uvivu na wivu. Walifaulu kuwashinda adui hao wote wakiitumaini tu neema ya Mungu. Basi, ikiwa hao ndugu zetu waliweza kufika Mbinguni, kwa nini hata sisi tusifike huko? Vita vinavyodumu kwa miaka michache hapa duniani, vitatuletea raha ya milele mbinguni.

Yafaa sana kuwaomba watakatifu, kwani wao ni marafiki wa Mungu. Mungu atawapa chochote kile wanachokiomba kwa ajili yetu. Wao wanatupenda sisi na wanatamani sana nasi tupate kuokoka. Hivyo, ikiwa sasa tunahangaika na kusumbuka, tusikate tamaa, yafaa tuiinue mioyo yetu juu tuzi-tazame mbingu jinsi zilivyo nzuri,na tuseme: "Enyi watakatifu wote, mtusimamie".

Maoni


Ingia utoe maoni