Marseli
Tarehe yenyewe aliyozaliwa Marseli haijulikani, lakini aliishi katika karne ya tatu. Alikuwa askari katika jeshi la Warumi. Alipoongoka na kubatizwa alijua kwa hakika kwamba hataweza kuendelea kuwa askari Mroma.
Wakati wa sherehe ya Kaisari Dioklesiano iliyofanyika mjini Tangiers (Moroko), Marseli aliutupa chini mkanda wake kijeshi, na kwa sauti kubwa akasema: "Mimi nitamtumikia Yesu Kristu, Mfalme wa Milele. Sitawatumikia makaisari wenu. Nadharau kuabudu miungu ya ubao na mawe, kwani ni vipofu na bubu". Askari wenzake wakashtuka kusikia maneno hayo, na kiongozi wa sherehe akatoa amri ya kumtupa Marseli gerezani. Baada ya sherehe akaletwa mbele ya baraza, akaulizwa maana ya kuutupa chini ule mkanda wake wa kijeshi. Akajibu hivi: "Mnamo tarehe 21 Julai, mbele ya bendera ya jeshi, nilitaja wazi kuwa mimi ni mkristu, na kwamba nitaweza kumtumikia Bwana tu, naye ni Yesu Kristu, Mwana wa Baba Mwenyezi". Fortunatus, mkuu wa baraza, akamwambia: "Siwezi kuusamehe ujinga wako. Kwa hiyo nitamwarifu Kaisari".
Basi, Marseli alipelekwa mbele ya maofisa wa daraja la juu zaidi ili ahojiwe. Akatoa majibu yale yale. Ofisa mkuu akamhukumu akisema: "Mwenendo wa Marseli unastahili adhabu kali, kwa kuwa alijishusha hadharani akitumia lugha ya kijinga. Basi, tumeamua auawe kwa kukatwa kichwa". Marseli alipopelekwa njea auawe, akamwambia Ofisa mkuu: "Na Mungu akubariki".
Maoni
Ingia utoe maoni