Alfonsi Rodriges
Alfonsi alizaliwa mjini Segovia (Hispania) mwaka 1531. Akiwa na umri wa miaka kumi na minne, alikwenda kufundishwa na mapadre Mayesuiti, lakini baada ya muda usio mrefu, akafiwa na babae. Ikaamuliwa kwamba ni afadhali Alfonsi arudi nyumbani akamsaidie mamae. Huyo mama alikuwa anajitahidi kuendeleza biashara ya sufu aliyokuwa ameirithi kwa hayati mume wake. Alfonsi alipofikia umri wa miaka ishirini na tatu, mamaye aliiacha kazi, na mambo yote yakawa chini ya madaraka ya Alfonsi, miaka mitatu baadaye alioa mke.
Baada ya kufiwa na mke wake, pia na mwanawe, aliomba ajiunge na Mayesuiti, lakini hawakumkubali. Alikaribia kuwa na miaka arobaini, afya yake ilikuwa si nzuri, na masomo aliyokuwa ameyapata zamani hayakumtosha aweze kusomea upadre. Alijaribu kujifunza kilatini pamoja na vijana, nao wakamcheka. Kwa sababu alikuwa amewapa dada zake na watu maskini hela zake karibu zote, akafanya kazi ya mtumishi wa nyumbani. Kwa kuwa mshahara wake ulikuwa mdogo mno, akalazimika kwenda kuombaomba.
Wakati huo alishawishika kuacha wazo la kujiunga na shirika la Mayesuiti, na badala yake aende akaishi katika upweke. Lakini akatambua upesi kwamba huo ulikuwa si wito wake, wala yalikuwa sio mapenzi ya Mungu kwake. Mwaka 1571 alikubaliwa kuwa bruda katika shirika la Mayesuiti, na miezi sita badaye akatumwa kufanya kazi katika chuo kilichokuwa kikiongozwa na Mayesuiti kisiwani Majorka katik Bahari ya Kati, si mbali ni Hispania, huko akawa mngoja mlango. Kazi hiyo ilihitaji uvumilivu wa hali ya juu, uthabiti na busara. Aliwapokea wageni wote walioingia katika Monasteri kama wangekuwa Yesu Kristu mwenyewe. Akakaa katika hali hiyo kwa muda wa miaka arobaini na mitano akiwatangulia watawa wenzake kwa mifano yake bora. Mara kwa mara wanafunzi wa chuo walikwenda kutafuta mwongozo kwa bruda Alfonsi, miongoni mwao Petro Klaveri (taz. 9 Septemba). Bruda Alfonsi alikufa mwisho wa mwezi Octoba mwaka 1617, akiyatamka kwa mapendo, majina ya Yesu na Maria. Alitajwa Mtakatifu mwaka 1888.
Maoni
Ingia utoe maoni