Bartolomayo wa Farne, Mtawa
Bartolomayo huyu alizaliwa mjini Whitby (Uingereza) uliopo Pwani ya Mashariki. Mwanzoni mwa karne ya kumi na mbili aliamua kusafiri mbali, na hivyo alifika katika nchi ya Norway ambako alikaa muda mrefu, akausomea upadre na kupadirishwa. Ndipo aliporudi nyumbani Uingereza. Wazee wake na wengine waliomfahamu walishangaa sana walipomwona amekuja akiwa padre. Bartolomayo akaondoka akajiunga na umonaki Durham (Uingereza) alipofanya kazi ya kiroho katika kanisa kuu la mji huo.
Husemwa kwamba alitokewa na Mtakatifu Kutibert wa Lindisfarne (tazama. 20 Machi). Mtakatifu huyu alimwambia Bartolomayo aende akaishi kama mkaa pweke kisiwani Farne, kilicho karibu na Pwani katika bahari ya Kaskazini. Abati wa monasteri ya Durham akamruhusu Bartolomayo kwenda kule. Hali ya hewa ya kisiwani ni baridi sana, mvua huwa inanyesha mara nyingi, na ukungu hukifunika kisiwa mara nyingi. Hapa Bartolomayo akawa mtakatifu na mfanya miujiza.
Kwenye kisiwa hiki Bartolomayo hakuishi peke yake, bali kwa muda tofauti alikuwa pamoja na wakaa pweke wawili wengine, na hakupatana na yule wa kwanza, aliondoka baada ya muda; yule wa pili, aligombana na Bartolomayo kwa sababu, alivyoona yeye, Bartolomayo alikula chakula kidogo mno; zaidi ya hayo, alisema mtu hawezi kula chakula kidogo hiki akaishi. Basi, akamshtaki Bartolomayo kwamba alikuwa ameficha mahali fulani, akiba ya chakula, ambacho alikuwa akikila usiku; kwamba alikuwa mdanganyifu na mnafiki.
Mashtaka hayo yalimuumiza sana Bartolomayo, kiasi cha kwamba atoke pale arudi Durham. Baadaye yule mkaa pweke mwenzake aliyebaki kisiwani, alisikitika mno, mara kwa mara akamwandikia akimwomba arudi Farne. Mwishowe Abati wa Monasteri ya Durham alimwamuru Bartolomayo arudi Farne. Alifanya vile, na waka pweke hawa wawili wakapatana kabisa, wakaishi kwa amani. Jinsi walivyofaulu kuishi hivyo ni jambo la ajabu kuliko miujiza aliyoifanya Bartolomayo.
Hizo ndizo habari za Mtakatifu ambaye aliyepigana vita kali sana ili aweze kuitimiza amri ya Yesu ya kumpenda mwenzake kama vile alivyojipenda mwenyewe. Alikufa kisiwani Farne, mwaka 1193, akazikwa palepale na wamonaki waliokuwa naye saa ya kufa kwake.
Maoni
Ingia utoe maoni