Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Jerome

Jerome

Mtakatifu Jerome, alizaliwa Machi 27, 342 katika mji wa Stridon Dalmatiae (Croatia ). Akaitwa Eusebius Sophronius Hieronymus. Akiwa na miaka 12, alisafiri kwenda Roma, kwa masomo, alijifunza uandishi, filosofia, kilatini na Kigiriki.Mwaka 366, mtakatifu Jerome, aliamua kuwa mkristo, akabatizwa na Papa Liberius.

Huko akaamua kusoma teolojia. Mtakatifu Jerome alisafiri kwenda Tier, akifuatana na rafiki yake aliyeitwa Bonosus, kutafuta elimu zaidi. Katika safari zake, alienda katika manosteri ya Aquileia, Italia mwaka 370. Manosteri hiyo ilikuwa chini ya Askofu Valerian, ambaye alikuwa mwenye busara mno. Hapo, Mtakatifu Jerome akakutana pia na Rufinus na wakawa marafiki . Rufinus alijulikana kwa umahiri wake wa kutafsiri maandiko ya Kigiriki kwa kilatini. Mtakatifu Jerome naye alikuwa na uwezo wa kutafsiri lugha tofauti pia.

Kutoka katika manosteri ya Aquileia, Mtakatifu Jerome alienda Treves, Gaul (Ufaransa ), ambako alitafsri vitabu mbalimbali kwa matumizi yake, akiwa na lengo la kuanzisha maktaba.

Mwaka 373, alirudi Aquileia, ambapo rafiki yake Bonosus aliamua kwenda kuishi pweke akitafakari makuu ya Mungu katika kisiwa cha Adriatic. Mtakatifu Jerome naye akasafiri kwenda Antiokia (Uturuki sasa), akipitia Athens (Ugiriki). Mwaka 374 mtakatifu Jerome alifika Antiokia, baada ya kusimama katika vituo mbalimbali. Akiwa huko alianza kuandika kitabu chake cha kwanza. Mwaka huo huo, mtakatifu Jerome, aliugua ugonjwa uliosababisha vifo vya wenzake kadhaa. Wakati akitaabika na ugonjwa, alipata maono mbalimbali, ambayo yalimuimarisha mno katika imani. Baadae naye aliamua kwenda kuishi jangwani, akiwa peke yake, ambapo alikaa kwa miaka 4.

Japokuwa mtakatifu Jerome aliporudi toka jangwani, aliendelea kuwa mtawa, akikaa pweke na kutafakari maandiko, lakini mababa wa kanisa, pamoja na Papa Damasus, walitaka awe padri. Mtakatifu Jerome aliomba endapo atakuwa Padri, basi aruhusiwe kuendelea na maisha ya kitawa na nyakati zingine aruhusiwe kwenda kukaa mwenyewe. Hivyo mtakatifu Jerome, akapata daraja la upadri. Akasafiri kwenda Constantinople (Istanbul Uturuki) ambako alienda kusoma kwa mtakatifu Gregory wa Nazianzus, ambaye alikuwa bingwa wa teolojia.Mwaka 382, Mtakatifu Jerome aliondoka Constantinople kwenda Roma, huko alionana na Papa Damasus. Papa alimtaka akae pale na awe Katibu wake. Papa Damasus alikufa mwaka 384 na Mtakatifu Jerome akabaki hapo.

Kutokana na misimamo yake ya ukweli, Mtakatifu Jerome akawa na maadui wengi na wakamtengenezea shutuma nyingi mbaya, na hivyo aliamua kuondoka Roma.Mwaka 386 alikwenda Antiokia na akaondoka hapo na kikundi cha waamini kwenda nchi takatifu. Mtakatifu Jerome aliendelea kuandika mafundisho mbalimbali kuhusu mama Bikira Maria na kutafsiri biblia kutoka kihebrania kwenda kilatini.

Mtakatifu Jerome alikufa tarehe 30 Septemba 420, kwa amani huko Bethlehem, Israeli.

Maoni


Ingia utoe maoni