Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Dorotea wa Montau

Dorotea wa Montau

Dorotea alizaliwa Montau (Ujerumani) mwaka 1347. Akiwa na umri wa miaka kumi na saba, aliolewa na mtu aitwae jina lake Alberto. Huyo alikuwa na tabia ya hasira kali sana, na kila mara alidai mambo yafanywe kama alivyotaka yeye. Dorotea alimzalia watoto tisa katika hao ni kitinda mimba wake tu aliyebaki. Aliteseka sana kwa ajili hiyo, na pia kwa ajili ya ukali wa mumewe.

Lakini kidogo kidogo, upole wake Dorotea pamoja na uhodari wake ulimbadilisha Alberto. Mwaka 1384, alimshawishi aende kuhiji pamoja naye, na kisha hapo walifanya mara nyingi. Wakiwa pamoja walipatembelea mahali kadhaa nchini Ujerumani wanapoheshimiwa Watakatifu mbalimbali. Wakaamua kwenda kuhiji Roma (Italia), lakini kwa bahati mbaya Alberto akaugua, na kwa hiyo, Dorotea akaenda peke yake. Aliporudi nyumbani alimkuta Alberto amekwisha fariki dunia.

Mwaka 1393 aliamua kuishi peke yake katika nyumba ndogo sana karibu na kanisa la Parokia mjini Marienwerder (Poland). Aliheshimiwa kuwa mtakatifu. Watu wengi walimwendea kuomba shauri au sala zake wapate kupona. Alikuwa na Ibada kubwa sana kwa Ekaristi Takatifu. Inasemekana kwamba pengine aliiona kwa namna ipitayo hali ya maumbile yetu. Lakini japo ya mambo mengi yaliyotukia maishani mwake ni ya ajabu mno, jambo la ajabu ni uvumilivu wake mbele ya tabia ngumu ya mumewe. Alifariki dunia mwaka 1394, na kwa muda watu wengi wa Prussia (Ujerumani Mashariki) walimwangalia kama mlinzi wao.

Maoni


Ingia utoe maoni