Jumanne. 30 Aprili. 2024

Mt. Mwenyeheri Benvenuta Bojani

Mwenyeheri Benvenuta Bojani

Alizaliwa mjini Kividale (Italia) mwaka 1254. Wakati wa utoto wake alionesha moyo wa Ibada kwa Bikira Maria, Moyo ambao ulikuwa wazi kwa kila mmoja aliyemwona. Aghalabu, kila siku, alisali sala ya "Salamu Maria" kwa namna ilivyokuwa desturi siku zile, yaani sehemu ya kwanza tu ya sala hiyo kama ilivyo hivi leo. Yasemekana kuwa maisha yake yote yalikuwa wimbo mmoja tu mfululizo wa sifa kwa mama Maria. Jamaa zake wote waliudhihirisha moyo huu wa kidini, na walifurahi Benvenuta aliopoamua kuweka nadhiri ya useja, na kujiunga na Utawa wa Tatu wa Mt. Dominiko.

Alijiwekea mazoezi makali sana ya nidhamu, kiasi kwamba, mwungamizi wake alikuwa hana budi kuingilia kati, na kumwamuru asifanye matendo yoyote ya kitubio pasipo kwanza kuidhinishwa naye.

Inasemekana kwamba alijifunga kamba kiunoni, akaikaza kabisa kiasi kwamba kamba hii iliingia ndani ya ngozi ambayo ilianza kuifunika hiyo kamba. Zoezi la aina hii lilimdhuru sana. Siku moja alimwomba Mungu amwepushe ili asihitaji operesheni, na kumbe, kwa ghafula, kamba ikadondokea chini.

Kwa muda wa miaka mitano, aliugua vikali. Mwenendo wake wa aina hiyo ulimletea mateso zaidi kuliko mazoezi ya Kitubio ya hapo zamani aliyokuwa amejichagulia yeye mwenyewe. Akashawishika kukata tamaa, hasa aliposhindwa kwenda kanisani kushiriki katika ibada ya Misa. Inasemekana kwamba siku moja alipona ghafula mbele ya watu wote waliokuwa wakisali. Aliwahi kuahidi kwamba pindi atakapopona, atakwenda kuhiji mahali pale alipozikwa Mt. Dominiko. Akaitimiza ahadi yake, akisindikizwa na dada na kaka yake.

Benvenuta aliuvumilia ukali wa vishawishi na maradhi, akazawadiwa fadhili nyingi za kiroho katika sala, kama, kwa mfano, alitokewa na mtoto Yesu katika utoto wake. Lakini, hatuna budi kukumbuka ya kwamba maishani mwake mambo makuu ni uchangamfu na matumaini yake katika ule muda mrefu wa ugonjwa wake. Na fundisho kuu jingine analotufundisha ni kuwa magumu na majaribio tunayoyapokea kwa Mungu, bila kulalamika, ni nafasi nzuri ya kumwitikia kwa upendo safi. Benvenuta alifariki dunia mwezi Octoba mwaka 1292. Wakuu wa kanisa waliruhusu ifanywe ibada rasmi kwa heshima yake mwaka 1765.

Maoni


Ingia utoe maoni