Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Yohani wa Kapistrano

Yohani wa Kapistrano

Yohani alizaliwa Kapistrano (Italia) mwaka 1386. Alijifunza sheria huko Perugia, na kwa muda, alikuwa hakimu na pia aliwahi kuwa gavana wa Perugia. Huko aliyatekeleza mambo yote kwa hekima na uadilifu. Watu walimsifu sana. Miaka minne tu baada ya kufunga ndoa, yeye na mke wake walikubaliana kutengana. Yohani aliona kuwa anasa za dunia na furaha zake si kitu, akavutwa kujiunga na utawa wa Mt. Fransisko. Kifungo cha ndoa kilipokatwa kwa ruhusa rasmi, akakubaliwa kuingia utawani, na mwaka 1420, akapadirishwa.

Utawani alionesha mfano wa kila fadhila, akisema daima: "Nimepata jina hili la Yohani ili nipate kuwa mfuasi mwaminifu wa Kristu na mtoto mpendwa wa Bikira Maria". Akaendelea katika kujikamilisha kiroho. Alijifunza sana teolojia, akamchukua Mt. Bernadini wa Siena (taz. 20 Mei.) kama mwalimu wake mkuu. Alikuwa mhubiri hodari sana, alitembea mahali pengi, akiwafundisha na kuwaongoza watu. Alihubiri katika nchi za Italia, Ufaransa, Ujerumani, Autralia, Hungaria na Poland.

Alijishughulisha pia katika harakati za kuleta mapinduzi katika shirika la Mtakatifu Fransisko, kwani maisha yao ya kiroho yalikuwa yametetereka. Vile vile alipewa jukumu la kuwaimarisha wakristu katika imani katoliki, na kuwapinga wazushi wa siku zile.

Baadaye, katika mwaka1455, Waturuki Waislamu waliwashambulia wakristu. Padre Yohani alihubiri vita vya msalaba dhidi yao, kwa ajili ya kuwaokoa wakristu. Juhudi zake huko Bavaria (Ujerumani) na katika Australia mwaka 1456 hazikufaulu sana. Punde Wagiriki wakaingia hata Belgrado (Yugoslavia). Padre Yohani alikazana zaidi kuhubiri ili wakristu waunde jeshi, na kupigana dhidi ya hao waturuki. Mwisho alikwenda vitani mwenyewe, akamfuata jemedari Hunyadi wa Hungaria, kusudi kuwatia moyo askari wakristu katika mapigano. Basi, wakristu waliuokoa mji wa Belgrado, na kisha wakawashinda waturuki. Hivyo Ulaya ya Magharibi iliokolewa siku hizo.

Baada ya vita, ulizuka ugonjwa kutokana na maiti nyingi zilizokuwa zimeachwa mjini bila kuzikwa. Padre Yohani alishikwa na Ugonjwa huo, akafa tarehe 23 Octoba mwaka 1456. Alitajwa kuwa mtakatifu mwaka 1724.

Maoni


Ingia utoe maoni