Jumanne. 30 Aprili. 2024

Mt. Margareta Klithero

Margareta Klithero

Alizaliwa mjini York (Uingereza) mwaka 1556, binti Tomas Middleton, liwali wa mji huo. Wazazi wake walikuwa Waprotestanti kama vile bwana John Klithero ambaye alimwoa Margareta akiwa na umri wa miaka kumi na mitano. Miaka mitatu baadaye akaongoka, akawa mkatoliki. Wakati ule dini ya kikatoliki ilikuwa imepigwa marufuku kabisa kufuatana na sheria za serikali ya Uingereza, na yeye aliyebainika akiishi kinyume cha sheria hiyo, alikamatwa na kupewa adhabu ya kifo. Margareta akiwa na umri wa miaka ishirini hivi, alikuwa mfurahifu na mwenye uso mzuri wa kupendeza. Kila mmoja alimkimbilia ili apate kusaidiwa, kutulizwa na kushauriwa naye. Akajulikana kama mkatoliki hodari asiyeogopa kusema wazi.



Basi, siku moja alikamatwa na kutiwa ndani kwa muda wa miaka miwili kwa kosa la kutohudhuria ibada katika kanisa la kiprotestanti. Wakati akiwa gerezani, alipata fursa ya kujifunza kusoma. Alipoachiliwa huru, alifungua shule ndogo ya nyumbani mwake ili aweze kuwafundisha watoto wake mwenyewe na wale wa jirani zake. Katika mahali pengine nyumbani mwake alikitayarisha chumba kidogo cha siri, nacho hakikuweza kugundulika ila kwa shida sana. Chumbani humu, aliweza kumficha padre aliyekuwa akija mara kwa mara kuwasomea Misa ili asije akakamatwa na polisi, wakamtesa vibaya na kumwua. Mume wake alifanya kana kwamba hakuwa na habari yoyote kuhusu mambo hayo.



Lakini, hata hivyo, siku moja aliitwa mahakamani ili aeleze mwanae alikuwa ameenda wapi. Kijana huyo, kinyume cha sheria za nchi, alikuwa ameenda ng'ambo kusomea upadre, jambo ambalo wakati ule, liliangaliwa kama tendo la uhaini kabisa. Basi, mapolisi wakaja kuipeleleza nyumba yake, bali hawakufaulu kukigundua kile chumba cha siri, wala padre, wala mavazi ya kanisa. Kila mmoja wa familia alihojiwa, lakini watoto hawakusema neno lolote, mwishowe mtoto mmoja asiye wa familia yao, alianza kuogopa, naye akawaeleza polisi kinaganaga.



Basi, Margareta akafungwa gerezani kwa mashtaka ya kuwaficha mapadre na kushiriki katika Ibada ya Misa. Akakataa kujieleza mintarafu mashtaka hayo akisema: "Sihitaji kuhukumiwa kwa kuwa sikutenda kosa lolote". Alifanya hivyo ili watoto na watumishi wake wasije wakalazimishwa kutoa ushahidi dhidi yake. Adhabu ya kukataa kujieleza baada ya mashtaka rasmi, ilikuwa ile ya kukanyagwa mpAka kufa. Hivyo, ndivyo alivyokufa Margareta Klithero mnamo tarehe 25 Machi 1586, akiwa imara katika imani yake. Mara kabla ya kuuawa alipiga magoti akasali. Watu waliokuwepo walistaajabu walipomwona akikunjua uso wake kwa furaha. Akasema kwa sauti: "Na Mungu ashukuriwe; yote anayonitumia nayapokea kwa shukrani; sistahili kifo kizuri kama hiki".



Miongoni mwa watoto wake, wawili walipadirishwa Ufaransa, na binti mmoja alijiunga na utawa katika nchi ya Ubelgiji.



Margareta alitangazwa mtakatifu katika mwaka 1970 kama mmojawapo wa wafiadini arobaini wa Uingereza.

Maoni


Ingia utoe maoni