Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Aloisi Gonzaga

Aloisi Gonzaga

Mtakatifu Aloisi Gonzaga, Somo wa vijana Wakristo alizaliwa mwaka 1568 na wazazi watukufu katika jumba la Kastiglione (Italia).

Alipokuwa na umri wa miaka mitano aliingia siku moja katika kambi ya askari akawasikia wakisema maneno yasiyofaa, naye aliyakariri maneno hayo, lakini bila kujua vema maana yake. Katika maisha yake yote Aloisi aliendelea kuijuta dhambi hiyo ndogo kama kwamba alikuwa amekosa sana.

Siku zote alikuwa na haya, kwa hiyo, hakutaka kutazama mwanamke usoni. Inasemekana kwamba kwa muda wa miaka miwili alikuwa akikaa katika mji wa Malkia, na wakati huo wote hakumwinulia macho hata mara moja. Kijana huyo Mtakatifu alipenda kushinda kutwa kucha mbele ya Sakramenti ya Takatifu ya Ekaristi. Kwa kulinda roho yake safi alikuwa akisali na kufunga. Alimpenda Mama wa Mungu kwa mapendo yasiyo na mfano.

Baba yake alitaka Aloisi awe askari. Lakini Aloisi alitaka awe Mmisionari, na hapo baba yake alikasirika sana. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na sita alijiunga na Shirika la Wajesuiti. Alihamia Roma (Italia) na huko akawapita wanafunzi wenzake kwa mfano bora. Mapadre wote walimsifu kwa kuwa hakuvunja sheria hata mara moja.

Furaha yake ilikuwa kuwafundisha Katekismu maskini na watu wa shamba. Aidha alipenda kwenda kuwatazama wagonjwa hospitalini. Zamani zile ulitokea ugonjwa wa kuambukiza mjini Roma, na Aloisi alipata ruhusa kwenda kuwatunza wagonjwa hao.

Baada ya muda yeye mwenyewe aliugua ugonjwa huo mkali, na kisha kupita muda kidogo ugonjwa wake ukazidi akapokea Sakramenti ya Wagonjwa, akafa mwenye kicheko cha furaha usoni mwake mwaka 1591, akiwa na umri wa miaka 23.

Aliandikwa katika orodha ya Watakatifu mwaka 1726.

Maoni


Ingia utoe maoni