Jumanne. 30 Aprili. 2024

Mt. Yohana XXIII, Papa

Yohana XXIII, Papa

Papa Yohane XXIII alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 huko Italia akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto 14 wa familia ya wakulima ya Giovanni Battista Roncali na Marianna Giulia Mazzolla. Jina lake la asili ni Angelo Giusseppe Roncali.

Alipewa daraja ya Upadre tarehe 10/8/1904. Wakati wa vita ya kwanza ya dunia, Padre Roncali alihudumu kama sergeant katika jeshi la Italia na chaplain tangu 1914 hadi 1918.Mwaka 1919 alikuwa mlezi wa kiroho seminarini. Katika nafasi zote hizi, padre Roncali alionesha upendo na unyenyekevu wa ajabu.

Mwaka 1925, mwezi Machi 19, aliwekwa kuwa askofu akichagua kama motto yake “unyenyekevu na Amani”. Kama askofu alihudumu katika nafasi mbalimbali kama Nuncio wa Ufaransa. Mwaka 1953 aliteuliwa kuwa Kardinali na papa Pius XII.

Roncali alichaguliwa kuwa papa tarehe 28/10/1958 akiwa na miaka 76. Kutokana na umri wake, wengi walimuita Papa wa mpito. Akiwa papa daima alipigania amani ya kweli duniani, ukweli uliojidhihisha katika barua yake Pacem in terris. Katika kuupigania usawa, papa Yohana XXIII daima alisisitiza “sote tuliumbwa katika sura ya Mungu, hivyo wote tu kama Mungu”. Papa alisema daima “hata kama Yesu anakutwisha msalaba, yupo kukusaidia kuubeba kwa sadaka na upendo”

Papa Yohana XXIII anakumbukwa zaidi kwa kuandaa na kuitisha Mtaguso Mkuu wa Vatikano II , mnamo tarehe 11/10/1962 uliojadili maswala muhimu juu ya Maisha ya Kanisa. Maazimio yake ndiyo yanafuatwa mpaka sasa.Anaitwa pia Papa mwema

Akiwa na miaka 81, papa Yohana XXiii alifariki dunia kutokana na kansa ya tumbo. Alitangazwa mtakatifu na Papa Francis tarehe 27/4/2014 .

Kutoka Maisha ya mtakatifu Papa Yohana XXIII tujifunze kuwa wanyenyekevu katika hali zote na kutumia vema karama zetu bila kujibakiza wala kujidharau, zaidi kukiongozwa na upendo na unyenyekevu unaoleta Amani.,Mfano, yeye katika uzee wake amelifanyia Kanisa jambo kubwa ambalo kamwe hatasahaulika.

Maoni


Ingia utoe maoni