Jumamosi. 04 Mei. 2024

Mt. Yohana Berkamans

Yohana Berkamans

Yohana Berkamans Mtawa
Yohani alizaliwa katika kijiji cha Diest (Ubelgiji) mwaka 1599, katika familia ya watu wenye kumcha Mungu. Baba yake alifanya kazi ya kushona viatu, lakini kazi hiyo haikumpatia masilahi ya kutosha. Hivyo Yohani aliyetaka kuwa Padre, baada ya kujifunza Kilatini kwa muda wa Miaka Mitatu, aliambiwa arudi nyumbani. Baba aliangaika sana kwa ajili ya kumtunza mke wake mgonjwa na Watoto watano, kiasi kwamba, kwa maoni yake, kumwona Yohani dukani kulikuwa bora zaidi kuliko kumwona, akiwa kama Padre, kwenye Altare lakini mwanae alimwambia:’’ Baba ,nitaponea maji na mizizi tu mradi niruhusiwe kuendelea na masomo yangu’’. Babake akamruhusu,lakini fedha za matumizi yake yote zilikuwa juu yake kuzitafuta. Basi,akajipatia kazi nyumbani kwa Padre mmoja na hivyo akaweza kujilipia ada ya shule.

Alipopata umri wa miaka kumi na sita, Mapadre Mayesuiti walimpokea katika chuo chao mjini Melkin (Ubelgiji), na Yohani mara akawapita wanafunzi wenzake wote kwa elimu. Baada ya muda si mrefu, aliomba ruhusa ya kuingi katika Shirika la Mayesuiti,nao wakamkubali. Juma moja kabla ya kuingia Utawa aliwaandikia Wazee wake:’’Baba na Mama, njooni kunitembelea niweze kuwaambia’Karibuni’ na ‘Kwa herini’,nanyi muweze kusema:’’Tunamrudishia Mungu mwana wetu ambaye tulimpata kwa kwa Mungu’’. Kisha kuingi katika Shirika la Mayesuiti, Yohani alionekana kuwa na fadhila nyingi na alifuata barabara kanuni ya Shirika. Nia yake Kuu ilikuwa kuitenda kikamilifu kila kazi ya kawaida. Alivyoona yeye,si kazi iliyokuwa muhimu bali namna ya kuitenda kazi hiyo. Namna zake hizo hazikumfanya awe mkavu, la,hata kidogo;bali aliwapendeza wenzake kwa kicheko na utani wake,akapata jina la kupanga’Frater Hilaris’maana yake ‘Ndugu Mchangamfu’.

Baadaye,wakuu wake walimpeleka Roma (Italia) ili apate kujifunza falsafa. Chumba alimokaa huko kilikuwa kilekile alimofia Mt.Aloisi Gonzaga. Yohani alifuata mfano wa mtangulizi wake katika kuuzingatia usafi wa moyo. Kabla ya kupadirishwa, alipatwa na ugonjwa mkali sana. Hakuonyesha dalili ya uchungu kufuatana na jambo hilo, bali alifurahi sana kupokea sakramenti ya wagonjwa. Aliwaomba mapadre walimtunza wampe mikononi kitabu cha Katiba ya Shirika, Rosari na Msalaba wake. Hatimaye aliyataja kwa furaha majina ya Yesu na Maria, na pale pale akafa mnamo mwaka 1621, akiwa na umri wa miaka ishirini na miwili tuu. Alitangazwa Mtakatifu mwaka 1888. Na Masalia yake yamo, pamoja na yale ya Mt. Aloisi Gonzaga, katika kanisa la Mt.Inyasi mjini Roma.

Maoni


Ingia utoe maoni