Padre Pio wa Pietrelcina
Mtakatifu Padre alikuwa ni mmoja kati ya watoto 8 wa baba Forgione na mama Maria, ambapo watatu kati yao walifariki wakiwa bado wadogo. Wazazi hawa walikuwa wakulima wadogodogo.
Mt. Padre Pio alizaliwa tarehe 25.05.1887 kusini mwa Italia katika mji wa Pietrelcina. Alipewa jina la Fransisko kwa heshima ya Mt. Fransisko wa Assizi. Familia yao haikuwa tajiri, lakini waliishi maisha yaliyojawa na utajiri wa mapendo na amani. Hawakuwa na vitu vya ziada, ingawa mama yao alijitahidi kuwahudumia na kuwatunza watoto vizuri.
Kwa moyo wake wa ukarimu, mama Maria alipenda daima kwenda kuchukua matunda shambani na kuyagawa kwa familia maskini. Jambo hili lilichangia sana kukuza fadhila ndani ya Fransisko Forgione. Familia hii kweli ilikuwa nyumba ya sala, kwasababu pamoja na mambo mengine, walizoea kusali pamoja sala ya Rozari Takatifu kila siku usiku kabla ya kulala.
Tangu utoto wake, Fransisko alionekana kuwa amejaliwa neema ya kuwa na vipaji vingi vya pekee na alikubalika kwa Imani yake thabiti, na moyo wa mapendo na bidii katika sala. Alijaliwa neema ya kuwaona Yesu Kristo na Mama Bikira Maria pamoja na Malaika wake mlinzi.
Alipokuwa na umri wa miaka 10, Fransisko alipata hamu ya kujiunga na Shirika la Ndugu Wadogo Wafransisko Wakapuchini. Mwaka huo huo alisikia mahubiri mazuri sana yaliyomfanya atambue uzito wa wito wake wa kuwa mtawa.
Kwa bahati nzuri, wakati huo akiwa bado na mvuto wa kuishi maisha ya kitawa, alitokea Ndugu mmoja jina lake Campillo (Mkapuchini) aliyetembelea huko Pietrelcina. Campillo aliishi vizuri sana fadhila za unyenyekevu na udogo. Mambo haya yalizidi kuamsha zaidi hamu ya Fransisko, hata akaamua kuwataarifu wazazi wake juu ya nia yake njema. Mara baada ya taarifa hiyo, wazazi wake walifanya kila namna inayowezekana ili kumsaidia mtoto wao atambue vema wito wake.
Mwaka 1903, alijiunga na shirika la Ndugu wadogo Wafransisko Wakapuchini huko Morcone na akachukua jina la Ndugu Pio kwa heshima ya Papa Pius wa v, aliyekuwa mtakatifu msimamizi wa mji wa Pietrelcina.
Alifunga nadhiri za kitawa mwaka 1907 na akapewa Daraja Takatifu la Upadre mwaka 1910. Daima Padre Pio alionekana akiwa katika hali ya unyenyekevu, tafakari, utulivu na mwenye moyo wa sala.
Upendo wake kwa Yesu wa Ekaristi, ulikuwa kama moto uwakao. Alizoea kusema “Ni rahisi dunia kuwapo bila jua kuliko kuwa bila Misa takatifu”. Alikuwa na upendo wa Pekee kwa mafukara, na daima alifanya bidii ya kutafuta wokovu wa wakosefu (wadhambi).
Misa nzuri iliyoadhimishwa na Padre Pio ilitumia muda mrefu kwasababu ya ukimya mrefu na tafakari ya kina. Alipoulizwa ni kwanini anatumia muda mrefu katika Misa Takatifu tofauti na Mapadre wengine, alijibu; “Mungu mwenyewe anajua kwamba nataka kuadhimisha Misa kama Mapadre wengine lakini nashindwa”
Padre Pio alikuwa na mazoea ya kuungama kila baada ya masaa 10 au 12, na alitumia muda wake mwingi zaidi kuungamisha. Mtu aliyetenda dhambi ya mauti aliondolewa na kusamehewa dhambi kwa Sakramenti ya Kitubio kupitia Padre Pio alisema; najisikia kama vile natembea hewani au naelea.
Kama ilivyokuwa utotoni, Padre Pio pia katika, maisha yake, aliendelea kupata mateso makali sana kwasababu ya afya yake iliyoanza kumsumbua tangu akiwa na umri mdogo. Pia alipata majaribu mengi na makali toka kwa shetani. Mara kwa mara shetani aliposhindwa kumwangusha Padre Pio katika dhambi alimwadhibu Mtakatifu huyo kwa mapigo mbalimbali makali. Pio alikimbilia msaada wa Malaika wake mlinzi pamoja na kwa Yesu na Bikira Maria wakati wa mapambano.
Tarehe 20 septemba mwaka 1918, Padre Pio akiwa amepiga magoti na kusali mbele ya Yesu msulibiwa, kama ilivyokuwa kwa somo wake Mt. Fransisko wa Assizi, Pio alipokea alama za Madonda Matakatifu toka kwa Msulibiwa. Madonda hayo yalidumu kwa muda wa miaka 50 hadi alipofariki dunia.
Daktari aliyemchunguza Pd. Pio alisema; “hakuna sababu yoyote ya asili iliyosababisha vidonda hivyo”. Vidonda hivyo havikuathiriwa na kitu chochote na wala havikupona, bali vilinukia kama mawaridi na kuvuja damu mpaka kifo chake. Pd. Pio Alipoulizwa kama alihisi maumivu yoyote ya vidonda, alijibu; ‘unadhani Bwana amenipa madonda haya kama mapambo?’.
Mbali na muujiza huu wa Madonda Matakatifu toka kwa Yesu msulibiwa, Pio alijaliwa pia zawadi ya unabii, uwezo wa kuonekana sehemu (eneo) zaidi ya moja kwa wakati mmoja (Bilocation), na uwezo wa kutambua mioyo ya watu hasa wakati wa kitubio. Kwa mfano mtu aliposahau au alipoamua kutotaja dhambi fulani kwa makusudi, Padre Pio alimweleza mtu huyo waziwazi na tena kwa ukali. Kwa hakika watu wengi walifaidi huduma yake.
Padre Pio alikuwa Padre wa kwanza kupewa zawadi ya Madonda Matakatifu. Kabla ya kufikisha umri wa miaka 30, alikuwa tayari amefikia hatua ya juu ya kiroho iitwayo Muungano. Alipendelea sana kusali sala ya Rozari Takatifu na alikuwa na upendo wa pekee kwa Yesu na Bikira Maria. Pia aliwahimiza sana waamini wengine kusali sala ya Rozari Takatifu.
Alizoea kuwaambia watoto wake wa kiroho hivi; “wanangu, rozari”. Alipenda na alisisitiza sana kuwaombea marehemu akisema; “Ni lazima tufanye toharani kuwa tupu kwa njia ya sala zetu”. Aliishi vema fadhila za kifransisko na maisha ya kujinyima, huku akifanya kazi ya huduma kwa muda wa masaa 19 akishughulikia wokovu wake na wokovu wa watu wengine.
Alifanikiwa kuwarudisha maelfu ya wanaume na wanawake katika Imani katoliki. Padre Pio hakusita kukemea jambo kwa msisitizo na kwa ukali alipoona yanatenedeka yasiyo sahihi.
Dada mauti (kifo) alimfika Padre Pio tarehe 23 septemba 1968 akiwa ameshika rozari mikononi kama ilivyokuwa kawaida yake. Maneno yake ya mwisho yalikuwa; Yesu Maria, Yesu Maria. Maneno haya aliyatamka mara kwa mara kabla ya kifo chake.
Baba mtakatifu Yohane Paulo II alimtangaza Padre Pio kuwa Mtakatifu tarehe 16 juni 2002, katika Misa ya kihistoria iliyohudhuriwa na watu wengi sana huko Vatkani. Kanisa huadhimisha kumbukumbu yake tarehe 23 Septemba kila mwaka.
Katika mwaka wa jubilei ya huruma 2016 – 2017, Baba mtakatifu Fransisko alipendelea sana kutumia mfano wa Mtakatifu Padre Pio, akiwahimiza Wakristo Wakatoliki kumwendea na kumrudia tena Mungu katika Sakramenti ya Kitubio.
Aliwahimiza sana Mapadre kuwa wajumbe wa huruma ya Mungu, kwa kufuata mfano wa Mtakatifu Padre Pio. Katika siku za uhai wake Padre Pio alisema; ‘Baada ya kifo changu nitafanya zaidi’. Pia aliongeza kuwa, utume wangu kamili utaanza baada ya kifo changu. Bila shaka alikuwa na maana ya kuwaombea wanadamu. Kwa hakika maneno haya yanadhihirisha ukweli wake mpaka sasa kutokana na watu wengi sana wanaopata na kufaidi msaada wa maombezi yake.
Huko San Giovanni Rotondo Italia, mahali alipoishi Mt. Padre Pio na sasa amezikwa, kuna kituo kikubwa sana cha hija ambapo inakadiriwa kwamba wanafika mahujaji zaidi ya million nane (8) kila mwaka. Kituo hiki ni ushuhuda mkubwa unaodhihirisha utukufu wa Mungu ndani ya Mtakatifu huyu na kinasaidia sana wongofu wa roho nyingi.
Maoni
Ingia utoe maoni