Kamili wa Lelis , Padre na Mwanzilishi wa Shirika
Kamili alizaliwa karibu na Chieti katika mkoa wa Abruzi (Italia) mwaka 1550. Mama yake alifariki mapema, yeye alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitatu. Kwa sababu ya kufiwa mapema na mamaye, alipotoka tabia akawa mvivu na mwasherati. Mwaka 1569, alipopata umri wa miaka kumi na tisa, aliingia uaskari pamoja na baba yake huve Venisi (Italia) wakati wa vita na Waturuki. Huko vitani yeye na baba yake walipatwa na ugonjwa. Babaye alikufa, yeye alipatwa na donda-ndugu mguuni, nalo liliendelea kumsumbua maisha yake yote.
Kamili alipenda sana kucheza kamari. Lakini katika kucheza kamari, alifilisiwa mali yake yote. Kwa sababu hiyo, ilimpasa kufanya kazi kwa Wakapuchini akisomba matofali ya kujenga nyumba. Alipoona kutokana na mwenendo safi wa mapadre Wakapuchini, alioushuhudia, naye akaongoka. Alizitupilia mbali furaha zake mbaya, akaziungama dhambi zake, kisha akawaomba mapadre hao Wakapuchini wampokee katika monasteri yao. Kwa sababu alikuwa na donda-ndugu mguuni, hakupata ruhusa ya kukaa humo. Alijaribu mara nne lakini alikataliwa tu.
Baada ya hapo alikwenda Roma, akaanza kuwahudumia wagonjwa katika hospital ya Mt. Yakobo. Siku zile huduma kwa wagonjwa katika hospital ziikuwa mbaya sana. Basi, Kamili alipoona watumishi wa hospitali hiyo wakiwatunza wagonjwa kwa uzembe bila kuwajali, alifanya shauri la kukusanya vijana ambao wangewatunza wagonjwa vizuri zaidi si kwaajili ya Yesu Kristu. Ilikuwa mwaka 1582 hivi, Kamili alipoanzisha shirika la kitawa la kuwahudumia wagonjwa hospitalini. Mwanzoni alipata migogoro mingi.
Kwa maongozi ya Mt. Filipo Neri; Kamili alipewa upadre mwaka 1584. Miaka miwili baadaye, Papa alilikubari shirika lake la wahudumu hospitalini, likaenea upesi nchini Italia. Wanashirika wanaitwa Wakamiliani. Ingawa Kamili alipata mateso mengi kwa kuugua, hakuchoka kuwatunza wagonjwa kwa upendo. Siku zake za mwisho, alipokuwa huko Genoa, ugonjwa wake ulimzidi sana. Alipokea mpako wa wagonjwa, akaaga dunia tarehe 14 Julai 1614. Alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1746. Yeye pamoja na Mt. Yohani wa Mungu na wasimamizi wa wagonjwa, na pia wasimamizi wa wauguzi na mashirika ya wauguzi.
Maoni
Ingia utoe maoni