Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Mt. Teresia wa Avila

Teresia wa Avila

Teresia alizaliwa Avila (Hispania) mnamo mwaka 1515. Wazazi wake walikuwa watu wa ukoo bora, na Wakristo hodari. Tangu utoto wake, Teresia, pamoja na mdogo wake Rodrigo, alipenda sana kusoma juu ya Maisha ya Watakatifu. Walivyoona hao wawili, wafiadini wakiteswa na kumfia Kristo walifaulu kuingia mbinguni kwa njia rahisi.

Kwa hiyo, licha umri wake mdogo wa miaka minane tu, Teresia alitamani sana kwenda Afrika ili apate kumfia Bwana katika nchi ya Waislamu. Lakini, kwa bahati mbaya, yeye na mdogo wake walipokuwa njiani wakielekea Afrika, mjomba wao aliwawahi, akawarudisha kwa mama yao aliyekuwa na hofu kubwa kuhusu watoto wake.

Teresia alifiwa na mama yake alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Akaenda kupiga magoti mbele ya sanamu ya Bikira Maria kumwomba ampokee kama mwanawe. Kutokana na kusoma vitabu vya hadithi za kipuuzi, Teresia akaelekea kulegea kidogo katika ibada, na kupenda umaridadi wa kila aina. Ndipo, baba yake alipompeleka akasome katika shule ya Masista ili wapate kumlea vizuri, lakini, baada ya mwaka mmoja na nusu, akaugua sana, ikabidi arudishwe nyumbani.

Alipopona, na kurudishiwa tena nguvu zake, Teresia akamwambia babaye kwamba alitaka kuwa Sista. Baba yake akamjibu akasema: "Baada ya kifo changu, utafanya utakavyo, lakini kwa sasa, hapana sikubali".

Alipopata umri wa miaka ishirini, Teresia alitoroka nyumbani akajiunga na konventi ya Masista Wakarmeli, akapewa jina la kitawa "Teresia wa Yesu", baba yake alipoipata habari hiyo, basi, akakubali tu.

Baada ya muda, Teresia akapatwa na homa kali ya Malaria iliyoendelea kumsumbua sana kwa muda wa miaka mitatu. Mwishowe, kwa kuwa daktari alidhani kwamba atakufa, akarudishwa kwao. Lakini, akapona, akarudi tena utawani, hata hivyo, tabia yake ikawa imebadilika kidogo.

Akaanza desturi ya kuzungumza sana na ndugu na rafiki zake katika chumba cha wageni cha konventi, na kuzungumza kidogo tu na Bwana Yesu, na kwa hivyo, hali ya utepetevu mwingi ilijipenyeza katika maisha yake ya kiroho, bali, baada ya muda, hususani kwa kusoma vitabu vizuri, akaanza, taratibu, kuugeuza mwendo wake tena, akakomaa kiroho na kusali vizuri zaidi.

Miaka ishirini na mitano tangu alipoingia utawa, akiwa amezoea kabisa kusali mara nyingi kwa kulingana na utaratibu uliowekwa, Teresia aliamua kuanzisha jumuiya ya Masista Wakarmeli walionuia kuishika, kwa uaminifu kabisa, ile katiba ngumu ya Wakarmeli kama ilivyokuwa hapo awali.

Masista wengi sana walikuwa wamekwisha zoea kuishi kufuatana na katiba ambayo tangu zamani kidogo, ilikuwa imeendelea kurahisishwa, na kwa hali hiyo, hawakutaka, kamwe marekebisho katika namna yao ya kuishi.

Lakini, Bwana Yesu mwenyewe alimtokea Sista Teresia, akampa moyo ili aendelee na jitihada yake. Basi, konventi ya kwanza ya Masista Wakarmeli wenye kufuata katiba iliyorekebishwa, ikafunguliwa mwaka 1562.

Wakati wa miaka ishirini iliyofuata Sista Teresia wa Yesu alikuwa akisafiri sana katika nchi ya Hispania akawahi kufungua nyumba kumi na saba za watawa waishio kulingana na katiba-rekebisho. Kwanza, kila Jumuiya ilikuwa na Masista kumi na watatu, baadaye, wakawa siyo zaidi ya ishirini na mmoja. Sala za pamoja, sala za binafsi na hususan sala za moyoni zilikuwa sehemu ya utaratibu wao wa kila siku; ruhusa ya kuongea ilitolewa kwa nadra, na kujinyima wasile nyama ndiyo iliyokuwa kawaida yao.

Mama Teresia, kama alivyoanza kuitwa, alikuwa siyo mwepesi kuwapokea wasichana waliokuwa wakimwomba kujiunga naye. Sharti la kwanza kabisa lilikuwa: awe na akili tambuzi yaani busara nzuri, kuliko kuwa na moyo wa ibada, kwa sababu, kama alivyoeleza Mama Teresia: "Mtu mwenye busara nzuri huweza kuyakiri makosa yake, huwa ni mnyofu, na yu tayari kuongozwa. Mtawa asiye na akili, hata anapoonyeshwa makosa yake, hayaoni; kwa hiyo, kamwe hataelewa kuyafanya yale yaliyotarajiwa kuyatekeleza; jinsi aonavyo yeye, na jinsi mambo yalivyo, kwake ni sawa tu. Hata kama Bwana wetu mwenyewe angemjalia moyo wa ibada na kumfundisha jinsi ya kufanya sala ya moyoni, ikiwa sista hana akili tambuzi, hangeneemeka kamwe, na badala ya kuwanufaisha wenzake, angekuwa mzigo tu, basi. Mungu atuokoe na Masista wapumbavu". Ndivyo Mama Teresia wa Yesu alivyofahamu.

Aliviandika vitabu vyenye mafundisho mazuri sana kuhusu maisha ya kiroho, navyo vinadhihirisha, kwa undani, hali halisi ya maisha yake mwenyewe ya kiroho. Barua zake nyingi ambazo zipo bado, zaonyesha kwamba, kwa tabia, alikuwa mpole, mchangamfu na mcheshi, aidha alikuwa na moyo wa upendo.

Alifariki dunia mwaka 1582, na mwaka 1622 akatajwa Mtakatifu. Miaka 350 baadaye, mnamo mwaka 1970, Mtakatifu Teresia wa Yesu, wa Avila, pamoja na Mt. Katarina wa Siena, alipewa heshima ya kuitwa Daktari wa Kanisa. Mpaka sasa ni Masista hao wawili tu waliopewa heshima hiyo.

Maoni


Ingia utoe maoni