Henriko, Kaisari wa Ujerumani
Henriko alizaliwa Regensburg mkoani Bavaria (Ujerumani) mwaka 973. Mtakatifu Wolfgang, askofu wa Regensburg, alimlea katika ibada na uchaji wa Mungu. Baba yake alipokufa aliirithi nchi ya Bavaria, akamwoa mke, jina lake Kunegunda.
Miaka kadhaa baada ya hayo, Henriko alichaguliwa kuwa Mfalme wa Ujerumani. Tangu siku ile, alifanya bidii kuistawisha dini katoliki katika nchi zake. Aliyajengesha upya makanisa mengi yaliyoharibiwa na maadui wa dini, akamrudisha Roma Papa Benedikto wa Nane, aliyefukuzwa na papa wa uwongo. Baba Mtakatifu naye alimwita aje Roma, akamvika kichwani taji la Ukaisari, kama tuzo kwa kazi zake njema za kumkinga Papa.
Kaisari Henriko, siku zote, aling'amua hatari zinazowanyemelea watu wanaokuwa katika madaraka makubwa. Kwa kusali aliweza kushika moyoni mwake fadhila za unyenyekevu na uchaji wa Mungu alizohitaji maishani mwake. Alifanya bidii kubwa kuleta amani na furaha katika milki yake, akasaidia kuwaongoa watu wa Hungaria wawe wakristu.
Alijenga kanisa kuu na monasteri mjini Bamberg. Kisha akaweka akiba fedha nyingi sana kwa ajili ya makanisa na maskini, kusudi ibada takatifu na huduma ya maskini viweze kuendelea mpaka mwisho wa nyakati. Alikufa mwaka 1024 akatangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1146.
Maoni
Ingia utoe maoni