Jumatatu. 06 Mei. 2024

Mt. Paulinus

Paulinus

Kanisa linafanya kumbukumbu kwa heshima ya Mtakatifu Pontius Meropius Paulinus aliyezaliwa mwaka 354 huko Bordeaux nchini Ufaransa.

Mtakatifu Paulinus alipata elimu yake huko Bordeaux na mara kadhaa alitembelea kituo cha Mtakatifu Felix huko Nola karibu na Naples.

Mtakatifu Paulinus akawa mwanasheria mashuhuri na kapata cheo kikubwa mjini Roma. Akaoa mwanamke aliyeitwa Theresia ambaye alikuwa Mhispania. Walipata mtoto ambaye alikufa mwaka 390.

Mtakatifu Paulinus aliamua kuacha mambo yote ya kidunia, akabatizwa na Mtakatifu Delphinus .

Akiwa na Theresia wakagawa mali zao kwa maskini na kwa kanisa.Wakaacha kila jambo wakaanza maisha mapya ya kikristo.

Mwaka 393 Mtakatifu Paulinus akapata Daraja Takatifu la Upadri na alipewa daraja hilo na Askofu wa Barcelona.

Akahamia karibu na kaburi la Mtakatifu Felix huko Nola nchini Italia. Yeye na Theresia walijaribu kuanzisha jumuia ya watawa.

Mtakatifu Paulinus akajenga hospitali, kanisa na basilica karibu na kaburi la Mtakatifu Felix.

Mtakatifu Paulinus aliteuliwa kuwa Askofu wa Nola mwaka 409.

Akafanya vema katika kazi yake, akawa na marafiki wengi. Na kwa kuwa alikuwa mshairi pia alitunga mashairi kumuenzi Mtakatifu Felix.

Mtakatifu Paulinus alikufa Juni 22, 431 huko Nola,Campania nchini Italia.

Maoni


Ingia utoe maoni