Jumanne. 03 Desemba. 2024

Mt. Philip Neri

Philip Neri

Mama Kanisa kwa namna ya pekee anatualika katika sikukuu kwa heshima ya Mtakatifu Philip Neri aliyezaliwa Julai 21, 1515 huko Florence nchini Italia. Baba yake Francesco di Neri alikuwa mwanasheria na Mama yake aliitwa Lucrezia da Mosciano.

Akiwa na miaka 18 Mtakatifu Philip Neri alipelekwa San Germano kwa mjomba wake aliyeitwa Romolo ili akamsaidie katika shughuli za biashara. Akafanya vema mno lakini akapata mwelekeo mpya wa kumfuata na kumtumikia MUNGU.

Mnamo mwaka 1533 alianza kufundisha katika sehemu tofauti na mwaka 1540 alianza kusoma masomo ya juu. Akaanza pia kuhubiri, kusaidia maskini na makahaba.

Akajiingiza katika kazi ya kuhubiri nyumba kwa nyumba na kwa miaka 17 alifanya kazi za kujitolea kama Mlei katika mji wa Roma.

Mwaka 1548 Mtakatifu Philip Neri alianzisha shirika kwa lengo la kusaidia mahujaji waliomiminika Roma na kusaidia wagonjwa waliotoka hospitali ambao hawakuwa na nguvu za kufanya kazi.

Mei 23, 1551 kwa neema ya MUNGU alipata Daraja Takatifu la Upadri. Akaamua yeye na wenzake kukaa katika Hospitali ya San Girolamo della Carita wakisaidia kazi mbalimbali.

Mwaka 1556 aliamua kuanzisha Shirika la Mapadre wa Wahudumu waliozunguka kuhubiri na kusaidia watu. Wakapata kibali cha Baba Mtakatifu mwaka 1575 na mwaka 1587 alichaguliwa kuwa Kiongozi wa kudumu wa shirika hilo jipya.

Mtakatifu Philip Neri alikufa Mei 25, 1595 huko Roma.

Akatangazwa Mwenyeheri Mei 11, 1615 na Baba Mtakatifu Paul V na 12 Machi 1622 alitangazwa kuwa ni Mtakatifu na Baba Mtakatifu Gregory XV.

Maoni


Ingia utoe maoni