Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Barnaba, Mtume

Barnaba, Mtume

Mtakatifu Barnaba alizaliwa katika kisiwa cha Kupros, na lugha yake ya kwanza ilikuwa Kigiriki. Mitume walimwita Barnaba maana yake 'mwenye kutia moyo'. Yeye hayumo katika idadi ya Mitume wale kumi na wawili, kama vile Paulo, lakini alipewa jina la Mtume tangu zamani, hasa kutokana na ushirikiano wake mkubwa na Paulo ambaye aliitwa Mtume wa Mataifa. Kanisa humuadhimisha kumbukumbu yake kama Sikukuu ya Mtume.

Inavyoonekana katika kitabu cha Matendo ya Mitume, Barnaba alivutiwa sana na mfano wa Wakristu wa huko Yerusalemu naye akaamua kuuza shamba lake na kuwakabidhi Mitume mapato yake. Alimsaidia Paulo, huyu alipopata shida baada ya uongofu wake kuonana na Wakristu wengine huko Yerusalemu, kwa sababu walikuwa wakimwogopa. Walimkumbuka bado kama mdhulumu wa Wakristu. Barnaba na Paulo walifanya safari za kimisionari kueneza Injili Antiokia (Siria). Kitabu cha Matendo chaeleza kwamba Barnaba alifanya kazi kubwa huko Antiokia na kusema juu yake kwamba "alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu" (Mdo 11:24). Baadaye walipitia nchi nyingine za Asia Ndogo (Uturuki): Kupros, Pamfulia, Likanomia na Kilikia (Mdo 13:2)

Barnaba na Paulo walikuwa na msimamo mmoja wakati shauri la Sheria ya Musa lilipotaka kuwatenganisha Wakristu. Wote walionyesha wazi kwamba hawakutaka kuwatwika mzigo wa sheria ya Musa wale watu wa mataifa ambao walimwamini Yesu.


Hatujui kwa hakika habari zaidi juu ya Barnaba, ila kadiri ya mapokeo aliendelea kuhubiri Injili katika kisiwa cha Kupros mpaka alipopigwa mawe na Wayahudi humo Salamina (Uturuki).

Maoni


Ingia utoe maoni