Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Mt. Landri, Askofu wa Paris

Landri, Askofu wa Paris

Mtakatifu Landri alikuwa askofu wa mji wa Paris (Ufaransa) zamani za Mfalme Klovis. Hatuna habari zake nyingi, ila alikuwa na huruma sana kwa wagonjwa na maskini. Yeye ndiye aliyeijenga ile hospital moja kubwa iliyoko Paris mpaka hivi leo, iitwayo Hotel-Dieu. Jina hili maana yake "Hospitali ya Mungu".

Mwaka mmoja ilitokea njaa kuu, Landri aliuza mali zake, akauza na vyombo vya nyumbani mwake apate kununua vyakula kuwapa watu wa mji. Njaa ilipozidi, kusudi watu wasife maana fedha zilikuwa zimemwishia, aliuza hata baadhi ya vyombo vitakatifu vya kanisa.

Ukarimu wake haukufa naye, kwa maana miujiza mingi ilitendeka kaburini pake. Wagonjwa walipokuwa pale kuomba, waliponywa. Siku moja ulizuka moto mkubwa katika mji wa Paris, nyumba nyingi zilianza kuwaka. Na watu walimkumbuka askofu marehemu baba yao, walikwenda wakatwaa sanda yake, iliyotunzwa tangu zamani katika kanisa ya Mtakatifu Jermano; wakaitia katika ncha ya ufito mrefu, wakaitandaza mbele ya moto. Mara ndimi za moto zilififia, na moto ukazimika.

Maoni


Ingia utoe maoni