Efrem, Shemasi na Mwalimu wa Kanisa
Mtakatifu Efrem alizaliwa katika nchi ya Siria, mnamo mwaka 306. Alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipobatizwa, akawa mwalimu wa dini baadaye. Aliendelea kujielimisha katika mafundisho makuu ya dini, akijificha mlimani, ili apate faragha ya kumwaza Mungu na kazi yake, na kuepa ushirikiano na watu. Lakini baada ya siku si nyingi utakatifu wake ulianza kujulikana, na hivyo, alitakiwa tena kwa kazi ya ualimu.
Alianzisha shule ya teolojia huko Edesa (Uturuki). Alipewa ushemasi, lakini walipomtaka awe padre alikataa kwa kuwa alijifikiria kwamba hastahili cheo hiki chenye ukuu na heshima. Alijitahidi kutoa mfano wa kila fadhila, hasa fadhila ya ibada na upendo kwa Bikira Maria.
Aliandika vitabu vingi vya kuwapinga walimu waliokuwa wakifundisha uwongo, na maandiko yake yalipata kuwarudisha watu wengi katika njia ukweli.
Umaarufu wake upo hasa katika hatuba zake, zilizoandikwa kama mashairi yafaayo kusomwa kwa sauti. Alitunga tenzi kwa ajili ya kuziimba. Nyimbo hizi zimejaa mafundisho, na Efrem alizitunga katika hali ya kuvutia watu kwa sauti nzuri, akapanga ziimbwe kanisani na kwaya ya wanawake. Insha zilizotungwa naye zinatumia mpaka leo kwenye makanisa ya Siria.
Alikufa mwaka 373 akiwa amejaa mastahili mengi. Mwaka 1920 Papa alimtaja kuwa Mwalimu wa Kanisa
Maoni
Ingia utoe maoni