Jumapili. 19 Mei. 2024

Mt. Yustini

Yustini

Mtakatifu Yustini Mfiadini alizaliwa na wazazi Wagiriki wapagani mjini Nablus katika mkoa wa Samaria (Palestina) mwanzo wa karne ya pili. Wazazi wake walimwelimisha. Alipata elimu kwa waalimu mashuhuri wa siku zile. Alikuwa mtaalamu katika falsafa, na alipoongoka aliandika vitabu vingi vya kutetea dini katoliki.

Yustini alipohitimu na kuwa mtu mzima aliona kwamba anajua mambo mengi isipokuwa mambo ya Mungu. Alijua kuwa Mungu ni Muumba, ni Mwenyezi, lakini kwamba mwanadamu anapaswa kufanya nini, haya hakuyajua. basi alianza kusoma maandiko ya wanafalsafa wakuu kama vile Sokrates na Plato. Hata vile hakuridhika. Mwisho aligundua kwamba ukweli juu ya Mungu unapatikana miongoni mwa Wakristu. Alianza kusoma Biblia na maandishi ya kikristu, na pia aliwauliza mapadre na viongozi wengine. Akayaelewa mambo ya Mungu. Hatimaye aliongoka, akabatizwa akiwa na umri wa miaka thelathini.

Alifika Roma na huko alifungua shule, na sifa za shule hiyo zilivuma kila mahali. Yustini alishiriki katika mabishano ya siku zile. Aliitetea dini ya kikristu, maana siku hizo, wakristu walikuwa wakiteswa na kuuawa ovyo kwa sababu ya imani yao. Yustini aliandika barua kwa Makaisari Antonini na Marko Aurelio akiwaonya waache kuwatesa wakristu. Katika barua hizo aliandika maneno yafuatayo: "Tunaposumbuliwa twaona furaha, kwa kuwa twaamini kwamba tukiuawa,Mungu atatufufua kwa ajili ya Yesu Kristu".

Ijapokuwa aliwatetea vile wakristu, Makaisari wa Roma hawakuilegeza amri ya kuwatesa wakristu. Yustini alishtakiwa kwa Kaisari Marko Aurelio, akatupwa gerezani, na baadaye akapelekwa mbele ya jemedari Rustiko. Alishurutishwa akane imani yake, lakini Yustini alikaa imara akisema: "Hakuna mwenye akili anayetaka kubadili ukweli kuwa uongo, Sisi ni wakristu; hatuwezi kutoa sadaka kwa miungu wa uongo".

Basi alihukumiwa kufa, mnamo mwaka 165.

Maoni


Ingia utoe maoni